Serikali ya Abdulswamad yajitenga na tamasha lililosababisha vifo baharini
SERIKALI ya Kaunti ya Mombasa imekanusha kuhusika na Tamasha la East African Oceanic iliyofanyika katika Mkondo wa Tudor wiki iliyopita, ambapo watu watatu walipoteza maisha.
Kwa sasa, uchunguzi wa mashirika mbalimbali kuhusu uwezekano wa dosari za usalama na ukiukaji wa kanuni za baharini unaendelea.
Gavana Abdulswamad Sheriff Nassir amesema ingawa serikali ya kaunti ilikuwa miongoni mwa wafadhili wa tamasha la kwanza la baharini lililofanyika 2024, mara hii haikuhusishwa kwa namna yoyote na makala ya mwaka huu, kwani yaliandaliwa na wadau binafsi.
“Tunathamini shughuli za kijamii kama hizi, lakini hafla hii haikuratibiwa na kaunti. Hakuna vibali vilivyotolewa. Naibu Gavana Francis Thoya alialikwa lakini kwa hekima yake akaamua kutojihusisha,” alisema Bw Nassir.
Aliongeza kuwa vyombo vya udhibiti kama Huduma ya Walinzi wa Pwani (KCGS) na Mamlaka ya Usalama wa Baharini (KMA) vitachunguza kubaini iwapo boti zilizotumika zilikuwa salama na iwapo washiriki walikuwa wamevaa mavazi ya usalama.
Gavana alizungumza haya baada ya miili ya watu wawili kati ya watatu waliozama kuopolewa Jumatatu alfajiri, kutokana na jitihada za siku nne za uokoaji na utafutaji.
Ajali hiyo ilitokea Oktoba 10 wakati wa mashindano ya mbio za boti, mojawapo ya shughuli za Oceanic Festival zilizofanyika katika Mkondo wa Tudor, Mombasa.
Kwa mujibu wa maafisa wa usalama, watu 22 walikuwa kwenye boti kadhaa wakati moja kati ya hizo ilipopinduka katika mazingira yasiyoeleweka.
Washiriki 19 waliokolewa, huku watatu wakitoweka.
Waliofariki wametambuliwa kuwa ni Steven Karembo, Tom Wanyonyi, na Caleb Otieno. Miili yao ilipatikana kati ya Daraja la Nyali na eneo la Jahazi Marine.
“Mwili mmoja ulipatikana karibu na eneo la ajali, huku miwili ikielea mbali zaidi,” alisema Bw Nassir.
Miili hiyo imechukuliwa na ndugu zao baada ya utambuzi rasmi na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Coast General (CGTRH).
Bw Nassir alieleza kuwa operesheni hiyo ilikuwa mojawapo ya juhudi kubwa zaidi za uokoaji tangu mkasa wa kivuko cha Likoni 2019, ikihusisha mashua 14 na zaidi ya watu 250 kutoka mashirika mbalimbali ikiwemo KCGS, KMA, Kenya shirika la msalaba mwekundu, na vikundi vya wavuvi (BMUs).
“Tumekuwa na siku ngumu sana. Hisia zilikuwa juu, lakini nawapongeza wote waliojitolea, hasa wanachama wa BMUs waliotoa mchango mkubwa katika uokoaji,” alisema gavana huyo.
Serikali ya kaunti kwa kushirikiana na serikali kuu zitaunga mkono familia za waliofariki kwa mipango ya mazishi, huku wanasaikolojia kutoka shirika la Msalaba Mwekundu na maafisa wa ustawi wa jamii wa kaunti wakitoa ushauri wa kisaikolojia kwa waathiriwa na jamaa zao.
“Kwa siku zijazo, timu za usalama na kikosi cha kukabili majanga cha kaunti lazima ziwepo kwenye matukio kama haya. Usalama si hiari,” alisema Bw Nassir.
Baada ya mkasa huo, timu ya usimamizi wa maafa ya kaunti imetaka kufanywe uchunguzi kamili chini ya uongozi wa Huduma ya Walinzi wa Pwani kubaini kilichosababisha ajali hiyo.
Uchunguzi huo utalenga hali ya usalama wa boti, uzingatiaji wa kanuni za baharini, na upatikanaji wa vifaa vya kuokoa maisha.
“Kwa kuepuka mkanganyiko, siku zijazo tamasha lolote la aina hii lazima lipate idhini kutoka kwa timu za usalama na maafa ya kaunti,” alisisitiza Bw Nassir.
Aidha, alitangaza mipango mipya ya kaunti kuhusu usalama wa baharini ikiwemo utoaji leseni kwa mabwawa ya kuogelea na ulazima wa kuwa na walinzi wa maisha walioidhinishwa.
“Mtu yeyote anayeendesha bwawa la kuogelea au shughuli za maji lazima awe na mlinzi wa maisha aliyehitimu. Tutatunga kanuni maalum kuhakikisha hilo linatekelezwa,” alisema.
Suluhisho la muda mrefu, idara ya Uchumi wa Bahari (Blue Economy) katika kaunti hiyo itaanza kuajiri na kufunza vijana kutoka BMUs kuunda kitengo maalum cha ukaguzi wa baharini, kitakachokuwa na jukumu la ukaguzi, usalama na uokoaji.
“Tunataka kuhalalisha vipaji hivi vya asili kwa kuwapa mafunzo na ajira za muda, huku tukishirikiana na KMA kupata boti maalum za ukaguzi na uokoaji,” alisema gavana huyo.
Alisema Bodi ya Utumishi wa Umma imeagizwa kuharakisha mchakato wa ajira, akisisitiza kuwa “usalama hauwezi kusubiri.”
Tamasha hilo la East African Oceanic Festival, lililovutia timu tisa zikiwemo Jeshi la Wanamaji la Kenya, Coast Guard, kikosi cha usalama kwa watalii, Chuo Kikuu cha Ufundi cha Mombasa (TUM) na makundi ya vijana wa pwani, limesitishwa hadi uchunguzi utakapokamilika.
Askari wamepelekwa eneo la Tudor Creek kuhakikisha usalama na kuzuia shughuli zisizoidhinishwa.
“Lazima tujifunze kutokana na tukio hili chungu. Hakuna maisha yanayofaa kupotea tena kwa uzembe au ukosefu wa kanuni,” alisema Bw Nassir.