• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 10:55 AM
Serikali ya Taita Taveta vitani kukomboa Mtito Andei na Mackinnon Road

Serikali ya Taita Taveta vitani kukomboa Mtito Andei na Mackinnon Road

NA LUCY MKANYIKA

SERIKALI ya Kaunti ya Taita Taveta imeagiza wafanyabiashara walioko katika miji yenye utata ya Mtito Andei na Mackinnon Road kulipa ada za leseni za biashara na mapato katika akaunti zake.

Haya yanajiri kufuatia uamuzi wa Mahakama Kuu uliopatia kaunti hiyo mamlaka ya kipekee kutoa leseni za biashara na kukusanya ushuru katika miji hiyo iliyoko katika kaunti za Makueni na Kwale mtawalia.

Kufuatia upinzani uliopita kutoka kwa wafanyabiashara na viongozi wa kaunti hizo, serikali ya Taita Taveta imeonya kuwa malipo yoyote ya ushuru au leseni yatakayofanywa kwa serikali hizo yatakuwa hasara kwa wenye biashara kwani watalazimika kulipa upya.

Serikali hiyo imeonya vikali wakazi na wafanyabiashara katika miji hiyo inayozozaniwa kuwa kutotii maagizo ya notisi hiyo kunaweza kusababisha hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi yao, ikiwemo kifungo kwa kukiuka amri ya mahakama.

“Wananchi, wafanyabiashara na wamiliki wa biashara wanahimizwa kufanya malipo yote kwenye akaunti zilizofunguliwa kabla au ifikapo tarehe 30 Machi 2024,” lilisema tangazo hilo lililotiwa saini na kaimu katibu wa kaunti Bw Habib Mruttu.

Mnamo Februari 2024, Mahakama ya Mazingira na Ardhi ya Mombasa ilipatia Kaunti ya Taita Taveta mamlaka ya kutoa leseni za biashara na kukusanya ushuru katika miji hiyo miwili.

Wafanyabiashara ambao hapo awali walifanya malipo kwa kaunti za Kwale au Makueni katika mwaka wa 2022 na 2023 kwa sasa wanahitajika kuwasilisha ushahidi kwa Kaunti ya Taita Taveta.

“Mtu yeyote atakayekiuka amri ya mahakama iliyotolewa tarehe 12 Februari 2024 atakuwa amedharau mahakama na atawajibika kwa kifungo kisichozidi miezi sita,” lilisoma tangazo hilo.

Notisi hiyo ilieleza kuwa maafisa wa ushuru wa kaunti watakagua biashara zote katika miji hiyo kuhakikisha kuwa agizo hilo la mahakama linatimizwa.

Jaribio la awali la serikali ya Taita Taveta kutekeleza ukusanyaji wa mapato katika miji hiyo lilikutana na upinzani kutoka kwa wafanyabiashara na viongozi wa kaunti hizo jirani.

Uamuzi wa mwaka 2023 ulijiri wakati Kaunti za Makueni na Kwale zilikuwa zimewashauri wafanyabiashara ‘wao’ kuendelea kulipa kodi kama kawaida.

Wakati huo huo, maafisa wa ushuru kutoka Taita Taveta walifukuzwa na baadhi ya wakazi wa miji hiyo walipojaribu kukusanya mapato katika miji hiyo yenye utata.

Baraza la Magavana liliingilia kati swala hilo ili kutafuta suluhu, na kuagiza Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) kuchunguza suala hilo.

Hata hivyo, Kaunti za Makueni na Kwale zimekata rufaa dhidi ya amri hiyo licha ya shinikizo la Taita Taveta kutekelezwa.

“Tumekata rufaa dhidi ya uamuzi huo na nataka kuwaambia kwamba hata inchi moja ya Makueni haitachukuliwa kutoka kwetu,” alisema Gavana Mutula Kilonzo Jnr wakati wa uzinduzi wa tarafa ya Kambu huko Makueni mnamo Machi 11, 2024.

Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki, aliyeongoza uzinduzi huo, aliwaagiza makamishna wa kaunti kutoka pande zote mbili kutatua suala hilo haraka na kutoa suluhu ndani ya wiki mbili.

“Lengo ni kufikia suluhu ya haki na yenye manufaa kwa pande zote ili kumaliza tatizo hili ambalo limezua mzozo kuhusu ukusanyaji wa mapato katika miji hiyo miwili,” alisema Prof Kindiki.

  • Tags

You can share this post!

Mapango ya hongo yaangaziwa katika ripoti ya EACC, Nyamira...

Serikali yasitisha zabuni za mashirika ya umma kukata...

T L