Habari za Kaunti

Siasa Pwani kuchukua mkondo mpya Joho akimleta kakake Abu kwenye mwangaza

January 20th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

SIASA za Pwani zinatarajiwa kuchukua mkondo mpya, Waziri wa Madini na Uchumi wa Baharini, Bw Hassan Joho na kakaye, Bw Abubakar Joho, almaarufu Abu, wakionekana kupanga mikakati ya kushawishi mwelekeo kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Joho ambaye amekuwa nguzo kuu katika siasa za ODM Pwani ameanza kujipanga awe ndani ya serikali ya kitaifa bila ushawishi wa aliyekuwa kinara wa ODM hayati Raila Odinga, huku chama hicho chenye mvuto kitaifa kikikumbwa na misukosuko.

Kwa upande mwingine, Abu ameonekana akihudhuria mikutano mbalimbali ya hadhara, tofauti na miaka ya awali ambapo alikuwa msiri.

Wiki iliyopita, wabunge wa Pwani chini ya muungano wao (CPG) waliandaa vikao kadha faraghani ambapo baadhi vilihudhuriwa na Bw Joho.

Ijapokuwa vikao hivyo vilidaiwa kuwa vya maendeleo, siasa za mustakabali wa Pwani 2027 hazikukosekana, suala lililobainika kwenye vikao na wanahabari.

Duru zimeeleza Taifa Leo kuwa waziri huyo ana machaguo kadhaa ikiwemo kupewa wadhifa wa uongozi ODM, kuwa kiongozi wa chama cha Pwani au kupewa wadhifa wa naibu kiongozi katika UDA.

Kwa njia yoyote ile, lengo ni kumwezesha Joho kuwa na usemi mkubwa katika maamuzi ya kuunda muungano 2027, au kupata nafasi itakayomwezesha kuwa uongozini katika serikali ijayo iwapo UDA itashinda urais.

Mbunge wa Kinango, Bw Gonzi Rai, alisema kufikia sasa Bw Joho amekuwa mtu muhimu katika kuwezesha wabunge wa Pwani kukutana na mawaziri au hata rais ili kujadili changamoto za wakazi, jambo ambalo lilikuwa vigumu hapo awali.

“Hivi majuzi tulimwambia tunahitaji kuzungumza na Waziri wa Usalama wa Ndani, Bw Kipchumba Murkomen, na akamleta. Tulifanya kikao cha faragha kwa kina kuhusu changamoto zetu, hasa utovu wa usalama. Mengine hatuwezi kufichua,” alisema Bw Rai.

Aidha, Bw Rai aliongeza kuwa Bw Joho amepanga mkutano mwingine na Waziri wa Elimu, Julius Ogamba, utakaofanyika hivi karibuni kujadili hali ya elimu Pwani.

“Tumekubaliana kuwa lazima tuwashirikishe pia Spika wa Bunge la Seneti Bw Amason Kingi na Waziri wa Spoti na Vijana Bw Salim Mvurya katika mikutano ijayo ili tusimwache mtu yeyote nyuma. Tunataka siasa za umoja na maendeleo,” alisema Bw Rai.

Bw Joho alianza kupata umaarufu kisiasa aliposhinda ubunge Kisauni katika mwaka wa 2007 hadi kuwa Gavana wa kwanza wa Mombasa kwa mihula miwili.

Mchanganuzi wa siasa Maimuna Mwidau, asema waziri huyo anatambua ushawishi wake unamweka pazuri kuwa nguzo muhimu kwa wanasiasa wanaolenga urais 2027, hasa Rais William Ruto.

Bi Mwidau aongeza kuwa, ingawa Rais Ruto tayari ana Spika wa Seneti Amason Kingi na Waziri wa Michezo Salim Mvurya upande wake, weledi wa kisiasa wa Bw Joho hauwezi kupuuzwa Pwani.

“UDA haikupata kura nyingi Pwani ndio maana wanalenga eneo hili. Bw Joho ni kiungo muhimu katika siasa za humu nchini. Licha ya kuwa Spika Kingi anashikilia nafasi ya tatu kubwa zaidi serikalini hawezi kumpiku Bw Joho kwa ufuasi na namna alivyoshikilia wabunge,” akasema.

Wakati Waziri Joho akishughulikia jinsi ya kusalia katika uongozi wa kitaifa, nduguye, Abu ameonekana akiunganisha siasa za Pwani.

Mikutano mingi anayohudhuria ni ya kulenga masuala ya vijana kuhusu ajira na pia kuwahamasisha kushiriki katika uchaguzi ujao.

“Tunamuunga mkono Bw Joho kama kigogo wa siasa za pwani na ni lazima awe kwenye meza ya kujadili maswala ya kisiasa na maendeleo ya kitaifa,” alisema Bi Getrude Mbeyu, Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Kilifi.

Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki Bw Suleiman Shahbal, alionya kuwa, endapo ODM itampuuza Bw Joho, wabunge wengi wa Pwani watamfuata akiamua kuondoka chamani.

Hata hivyo, Mbunge wa Nyali Bw Mohammed Ali ndiye kiongozi pekee ambaye amekuwa akikashifu hadharani Bw Joho na nduguye kwa ‘kuteka’ nyara uongozi wa Mombasa.