Siaya: Kaunti ambayo MCAs ‘wamebobea’ kutimua viongozi wakuu serikalini
BUNGE la Kaunti ya Siaya sasa limegeuzwa uwanja wa sarakasi huku madiwani wakiwasilisha hoja ya kuwatimua mawaziri katika utawala wa Gavana James Orengo wakati ambapo bunge lenyewe limekashifiwa kutokana na utendakazi duni.
Waziri wa Biashara Grace Agola ndiye wa hivi punde kujipata pabaya baada ya Diwani wa Ugenya Mashariki Fredrick Omoro kuwasilisha hoja ya kumtimua.
Mnamo 2023, Naibu Gavana William Oduol alitimuliwa na bunge la kaunti lakini akaokolewa na Seneti.
Naye aliyekuwa Waziri wa Maji Dkt Julie Onyango aliondolewa madarakani pia mwaka huo kupitia hoja hiyo hiyo ya madiwani.
Bunge la kaunti sasa limekashifiwa na mashirika ya kijamii, wanawake na viongozi wa kisiasa ambao wanadai kutimuliwa kwa viongozi ni njama ya madiwani kuwafumba macho kisha kujitajirisha kisiasa.
Chris Owala, ambaye ni Afisa Mkuu Mtendaji wa Shirika la Kijamii la CIAG-K amesema kuwa madiwani wanatumia hoja za kuwatimua mawaziri kwa manufaa yao ya kibinafsi.
“Timuatimua za kila mara zimeweka mazingira mabaya ya utendakazi na raia nao hawapati huduma,” Bw Owala akasema kupitia taarifa Jumatatu, Aprili 7, 2025.
“Hili suala limeingizwa siasa za kieneo kwa sababu juhudi zinazoendelea za kumtimua Bi Agola na kuondolewa mamlakani kwa Dkt Julie Onyango zote zilielekezwa kwa wanaotoka eneobunge la Alego Usonga.
Aidha, Bw Owala alisema kuwa kulengwa kwa viongozi wanawake kunakiuka usawa wa kijinsia na kuwadhalilisha wanawake wanaoshikilia vyeo hivyo.
Zaidi ya madiwani 30 wametia saini hoja ya kumtimua Bi Agola ambaye wanasema amelemewa kutekeleza majukumu yake na pia anadaiwa kukiuka Katiba.
“Waziri wa Biashara Grace Agola amelemewa kutekeleza majukumu yake ipasavyo na kwa njia inayoeleweka,” ikasema hoja hiyo.
Anadaiwa alikataa kuwasilisha stakabadhi muhimu kwa kamati ya bunge ambayo imekuwa ikichunguza uajiri kwa njia isiyofaa ya vibarua na wale wanaodumisha usafi kwenye masoko mbalimbali.
Baadhi ya wanachama wa kundi la Maendeleo Ya Wanawake na wakazi wa Siaya, wamemtetea wakisema anaandamwa kwa sababu za kisiasa.
Bi Rosemary Ogutu, mwanachama, alisema kuwa mwenendo ambao wanawake wa Siaya wanalengwa na bunge la kaunti limesawiri asasi hiyo vibaya.
“Kile kinachojitokeza ni kuwa wanaume hawafurahii uongozi wa wanawake na tunawaomba madiwani wetu wa kike wasikubali kuingia kwenye mtego huu,” akasema.
Bw John Ogeya kutoka vuguvugu la SCAN Siaya alilalamika kuwa hoja za kuwatimua maafisa wa kaunti zimelenga tu wale wanaotoka eneobunge la Alego Usonga.
“Naibu Gavana Oduol, Dkt Julie na sasa Grace Agola wote wanatoka Alego Usonga na tunahisi jamii yetu inalengwa,” akasema Bw Ogeya.
Mbunge wa Alego Sam Atandi naye hivi majuzi alikosana na Gavana Orengo kuhusu kubuniwa kwa serikali jumuishi.