Habari za Kaunti

Sita walioangamia kwenye maporomoko Murang’a wazikwa

May 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANGI MUIRURI

MBUNGE wa Kiharu Ndindi Nyoro mnamo Ijumaa aliongoza waombolezaji kuwapa heshima za mwisho watu sita wa eneobunge la Mathioya waliofariki baada ya kuzikwa wakiwa hai na maporomoko ya ardhi mnamo Aprili 30, 2024.

Gavana wa Murang’a Bw Irungu Kang’ata hakufika katika mazishi hayo.

Waombolezaji walivaa nyuso za huzuni kwenye ibada kabla ya mazishi, ikizingatiwa kwamba wote walikuwa wa familia moja.

Wahanga hao kutoka kijiji cha Kiganjo walizikwa na mchanga uliokatika na kisha ukawafunika wakiwa wamelala majumbani mwao mwendo wa saa saba usiku.

Majeneza yenye miili ya wahanga sita wa maporomoko. PICHA | MWANGI MUIRURI

Watu wengine 12 waliponyoka mauti huku zaidi ya 50 wakifurushwa makwao na kuwa wakimbizi wa ndani katika kambi ya Shule ya Msingi ya Ngutu.

Ni janga lililotokeza wazi uhasama wa kisiasa kati ya Bw Nyoro na Naibu Rais Rigathi Gachagua walioshindania kufika mahali hapo kutoa rambirambi zao.

Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro akiwasili Mathioya kwa ibada kabla ya mazishi ya wahanga sita wa maporomoko. PICHA | MWANGI MUIRURI

Rais William Ruto alizuru Kaunti ya Murang’a mapema Ijumaa lakini hakufika katika mazishi hayo.

Badala yake akiandamana na Bw Kang’ata, alifika katika msitu wa Kawaharura kupanda miti na kukumbuka waathiriwa wa janga la mafuriko linalokumba nchi.

Bw Nyoro akiandamana na mfuasi wake sugu katika siasa za ubabe wa Mlima Kenya ambaye ni Seneta wa Murang’a Bw Joe Nyutu. Wengine waliofika katika mazishi hayo ni Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Murang’a Betty Maina, Mbunge wa Kigumo Joseph Munyoro, Mbunge wa Mathioya Edwin Mugo, mwenzao wa Kandara Chege Njuguna na Waziri wa Vijana, Spoti na Utamaduni wa Kaunti ya Murang’a Manoah Gachucha.

Baadhi ya viongozi walioandamana na Ndindi Nyoro. PICHA | MWANGI MUIRURI

Ni mbunge tu wa Maragua Mary wa Maua ambaye hakufika katika mazishi hayo, hali inayoashiria taswira kamili ya wanamirengo katika miereka hiyo ya ubabe.

Wanasiasa wengine wa Murang’a ambao hawakufika katika mazishi hayo ni Seneta Maalum Veronica Maina na Mbunge Maalum Sabina Chege.

Katika hotuba zao, wanasiasa hao walielezea umuhimu wa umoja wa watu wa Murang’a na taifa kwa ujumla.

Walisema umoja ndio tu unaoweza kuwapa maendeleo ya haraka kutoka kwa serikali ya Rais Ruto na kujihakikishia makuu katika siasa za siku za halafu.