Tahadhari: Samaki kuwa adimu, mazingira Ziwa Victoria yakiendelea kuchafuliwa
GEORGE ODIWUOR Na WANDERI KAMAU
WAVUVI kutoka eneo la Nyanza wanalalamikia kupungua kwa kiwango kikubwa kwa samaki katika Ziwa Victoria.
Kwa miaka mingi sasa, kiwango cha samaki wanaovuliwa katika ziwa hilo kimekuwa kikipungua, hali inayotishia upatikanaji wa chakula cha kutosha na hali ya maisha ya mamia ya watu wanaotegemea samaki katika kaunti za Kisumu, Siaya, Homa Bay na Migori.
Kwa sasa, Kaunti ya Homa Bay ndiyo huwa inazalisha kiwango kikubwa zaidi cha samaki. Kaunti hiyo pia ndiyo yenye ufuo mrefu zaidi wa ziwa hilo.
Kulingana na idara ya kusimamia uvuvi katika kaunti hiyo, Homa Bay huwa inazalisha tani 52,000 za samaki kila mwaka.
Hata hivyo, kiwango hicho ni cha chini ikilinganishwa na mwongo mmoja uliopita, ambapo kaunti ilikuwa ikizalisha tani 70,000 za samaki kila mwaka.
Mkurugenzi wa Uvuvi katika kaunti hiyo, Bw George Okoth, alisema kuwa, samaki hao ni wale wanaovuliwa ziwani pekee.
“Baadhi ya samaki wanaouzwa ni wale waliofugiwa kwenye vyumba maalum vya kuwafugia samaki. Ni hali inayotusaidia kukabili upungufu uliopo wa samaki,” akasema.
Bw Okoth alionya kuwa kiwango cha samaki wanaovuliwa kutoka ziwa kitapungua hata zaidi, ikiwa hakuna hatua zitakazochukuliwa kudhibiti hali hiyo.
Moja ya hali zinazopunguza kiwango cha samaki wanaovuliwa kutoka ziwa ni uharibifu wa mazingira.
Wataalamu wa mazingira wameonya kwamba ikiwa hakuna hatua za haraka zitakazochukuliwa kukabili uharibifu wa maji, basi hilo litasababisha baadhi ya aina za samaki kuisha katika ziwa hilo.
Waliziomba familia zinazoishi kwenye fuo za ziwa kushiriki kwenye shughuli zinazolenga kulilinda dhidi ya uharibifu.
Walisema kuwa ziwa hilo linaendelea kukabiliwa na tishio la uharibifu, hali itakayowaathiri viumbe wengi.
Hivyo, aliomba uwepo wa juhudi za pamoja katika kulinda ziwa hilo dhidi ya aina tofauti za uharibifu.
Maafisa kutoka Vuguvugu la Uhamasishaji la Ukanda wa Ziwa (LREN), waliongoza zoezi za usafishaji mazingira katika Ufuo wa Wadiang’a, mjini Sindo, ambako walieleza hofu yao kutokana na kiwango cha juu cha uharibifu wa ufuo huo.
Zoezi hilo lilifanywa ili kuihamasisha jamii kuhusu uharibifu unaoyakumba maji kote duniani.
Mkurugenzi wa vuguvugu hilo, Bw Samuel Masiwo, alisema kuwa ongezeko la kiwango cha uharibifu katika ziwa hilo ni miongoni mwa sababu ambazo zimekuwa zikichangia mkurupuko wa magonjwa na kupungua kwa kiwango cha samaki.