Habari za Kaunti

Taharuki yatanda Mwingi Kaskazini mkazi akiuawa

Na  Boniface Mwaniki  March 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

TAHARUKI imetanda katika eneo la Ngomeni, eneobunge la Mwingi Kaskazini katika kaunti ya Kitui, baada ya wafugaji wanaoshukiwa kuwa wa asili ya kisomali kumuua mkazi mmoja.

Tukio hilo lilitokea mnamo Jumatatu, hata baada ya serikali kuajiri polisi wa akiba ili kudumisha usalama katika maeneo hayo ya mpakani wa Kitui na kaunti ya Tana River.

Akithibitisha tukio hili, Mkuu wa polisi wa wilaya ya Kyuso,  Samson Rukunga, alisema kuwa idara ya polisi imeanzisha uchunguzi mara moja ili kubaini waliotekeleza mauaji haya.
“Ni kweli kuna mtu aliyeua Jumatatu katika maeneo ya Kasiluni pande za Ngomeni. Tayari maafisa wetu wamo mbioni kuwatafuta washukiwa wa mauaji haya, huku uchunguzi wa mwanzo ukibaini kuwa ni wafugaji wasili ya kisomali,” alisema Bw  Rukunga.

Hata hivyo, Bwana Rukunga alikana madai kuwa marehemu aliuawa kwa kupigwa risasi, akisema kuwa uchunguzi wa mwili wake ulidhibitisha kuwa aliuaa kwa kukatwa kwa panga.

“Uchunguzi wa majeraha kwenye mwili wake yalibaini kuwa marehemu alikufa baada ya kukatwa kwa panga,” alieleza Mkuu huyu wa polisi.

Kulingana na wakazi, wafugaji  hao walimpata marehemu kwenye msitu, alipokuwa akichoma makaa pamoja na wenzake wanne. Baada ya kufumaniwa, wanne hao walitoroka na kumwacha marehemu aliyeuawa kwa kupigwa risasi.

Akizungumza na Taifa Leo, Mbunge wa Mwingi Kasikazini  Paul Nzengu ameitaka serikali kuchukua hatua dhidi ya waliohusika na mauaji ya juzi na kuwapa nguvu askari wa akiba (NPR) Ili kudumisha usalama ipasavyo.

“Hatuwezi kuruhusu mauaji ya kiholela kurejea katika eneobunge letu. Serikali inafaa kuwachukulia hatua kali waliotekeleza mauaji haya,” alisema Bw Nzengu.

Hata hivyo, mbunge huyu alilalamika kuwa askari wa akiba walioajiriwa wamepokonywa uwezo wa kudumisha usalama katika maeneo ya mpakani akidai wameamrishwa kutochukua hatua kali kama kutumia bunduki zao, wakati wa uvamizi.

“Kuna tetesi kuwa askari wa akiba walioajiriwa wameamrishwa wasichukue hatua yoyote hata wakati maafa yanapotendeka. Kutowapa nguvu askari hawa kunachangia pakubwa uvamizi wa mara kwa mara katika maeneo haya,” alieleza Bw Nzengu.

Sasa wakazi wa maeneo haya ya Ngomeni wanaiomba serikali kuingilia kati, Ili kuzuia hali ya ukosefu wa usalama.