Habari za Kaunti

Tana River hakukaliki kwa joto kali usiku na mchana

January 9th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA STEPHEN ODUOR

WIKI chache baada ya kukumbwa na athari za mafuriko kutokana na mvua ya El-Nino, wakazi katika Kaunti ya Tana River sasa wanakabiliana na hali ya joto kali mchana na usiku vile vile.

Mchana, jua linachomoza kwelikweli, kiwango kikifika nyuzijoto 40 nayo usiku kiwango ni nyuzijoto 30 kwa kipimo cha sentigredi.

Wakazi sasa wanafanya kila wawezalo kutafuta mbinu za kustahimili hali hii.

Wakati wa mchana, wengi huacha kufanya kazi na kuhamia chini ya miti na vivuli vingine, huku wengine wakijimwagia maji mfululizo ili kupoza joto kali.

“Wakati mwingine unahisi moto unawaka chini ya nguo zako, unajisikia kutembea uchi lakini ukifikiria joto unalopata kwenye ngozi yako, unasahau mawazo hayo,” alisema Maulidi Juma, fundi wa ujenzi.

Kulingana na Bw Juma, nguo zinapokuwa na unyevu husaidia kupoza joto jingi.

“Katika kazi hii, unaweza uazimia mwisho wa siku. Wengine wameachana na kazi, mimi ni mwajiriwa mpya,” alisema.

Saa saba mchana, mji wa Hola hubadilika kutoka asili yake ya kawaida yenye shughuli nyingi hadi eneo lisilo na watu.

Wafanyabiashara hukimbia jua wazi na kujificha katika maduka, wakati wengine huchagua vivuli vya miti.

Mavazi hubadilika ghafla, wanaume wakijifunga kikoi kiunoni na kuvaa kaptula huku wanawake wakichagua nguo nyepesi kama vile dera.

“Njia pekee ninayoweza kutegemea ni kuvaa nguo nyepesi na kunywa maji mengi, huwezi hata kutumia mafuta kwa ngozi yako kwa sababu inaleta madhara zaidi,” alisema Saida Fateh, mfanyabiashara.

Waendesha bodaboda hutoroka kazini mwendo wa saa saba mchana wakati joto liko juu zaidi. Wengi wao hupata kivuli cha kujificha kutokana na jua kali, huku wengine wakikimbilia mtoni.

Usiku, wakazi huweka mikeka nje. Kuna joto lakini kuna upepo kidogo, kwa hivyo wanalala nje.

Kwa mujibu wa Dhahabu Hassan, mkazi, nyumba ina joto kali sana kwao, hivyo wanalazimika kufanya mipango ya kulala nje.

“Imetufanya kutelekeza vitanda vyetu ambapo tunaweka mikeka na kuzungusha eneo hilo kwa neti za kuzuia mbu. Huko ndiko tunakolala hadi asubuhi,” alisema.

Kulingana na wakazi, hali hii imewasababishia baadhi yao hasa watoto tatizo la harara kwenye ngozi.

Afisa wa utabiri wa hali ya hewa katika kaunti, Bw Kalu Nyale, alisema joto jingi ilitarajiwa wakati huu baada ya msimu wa mvua.

Aliwashauri wakazi wajiepushe kukaa au kutembea kwa jua kwa sababu inaweza kuwasababishia madhara na badala yake wawe wakitafuta kivuli.

“Pia unywaji maji mengi na kuoga kwa maji baridi inaweza kusaidia,” akasema.

Aliongeza kuwa, hali hiyo inaweza ikaendelea hadi mwisho wa Februari au Machi.

Kaunti nyingine za Pwani pia zimekuwa zikishuhudia joto jingi tangu katikati ya mwezi wa Desemba, ambapo joto limepanda hadi kati ya nyuzijoto 28 na 30.