Habari za Kaunti

Tulitaka ‘kumsalimia’ Gavana wetu Timamy lakini hayupo; tutarudi akija – Gen Z wa Lamu

Na KALUME KAZUNGU July 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

VIJANA wa kizazi cha Gen Z Kaunti ya Lamu Jumanne walikatiza maandamano yao nyakati za mwisho mwisho baada ya kugundua kuwa Gavana Issa Timamy hakuwa ofisini.

Mamia ya vijana hao wiki jana walikuwa wametangaza mpango wao wa kuvamia makao makuu ya kaunti ya Lamu, mjini Mokowe Jumanne wiki hii katika kile walichokitaja kuwa ni kutafuta haki.

Walikuwa wameeleza kuwa dhamira kuu ya kufika kwenye makao makuu ya kaunti ya Lamu ni kumuona na ‘kumsalimia’ Gavana Timamy na kumshinikiza kutimiza matakwa yao.

Miongoni mwa matakwa ambayo Gen Z wa Lamu wanashinikiza kutekelezwa na serikali hiyo ya kaunti ni, kufutiliwa mbali kwa mamilioni ya fedha yanayotumiwa kufadhili Tamasha za kila mwaka za Utamaduni wa Lamu.

Gen Z wanataka fedha hizo zitumike kutekeleza miradi ya maendeleo ambayo ni ya kumnufaisha mwananchi wa kawaida.

Mbali na tamasha za utamaduni wa Lamu, Gen Z wa eneo hilo pia wanataka kaunti kurejesha mara moja mfumo wa basari kwa wanafunzi wanaosoma vyuo vikuu, kufutiliwa mbali kwa bajeti ya fedha za umma zinazotumika kufadhili ziara za nje ya nchi kwa mawaziri wa serikali ya kaunti na pia Bunge la Kaunti ya Lamu miongoni mwa masharti mengine mengi.

Vijana waandamana Lamu wakimtaka Gavana wao atimize makataa yao. picha| Kalume Kazungu

Katika mahojiano na Taifa Leo Jumanne, aidha, vijana wa hao walisema waliafikia kusitisha maandamano yao hadi pale Bw Timamy atakapokuwa ofisini.

Mmoja wa vijana wa Gen Z, Bw Mohamed Omar alisema katu hawawezi kwenda kwa makao makuu wakiandamana ilhali yule wanayetarajia kukutana naye akiwa hayupo.

“Azma ya maandamano yetu ni kumuona na ‘kumsalimia’ vyema Gavana Timamy. Kuna masharti mengi tulitoa wiki moja iliyopita, ambapo tulipeana makataa ya siku saba ambayo yameisha leo. Tulitaka sana kuandamana lakini kwa vile gavana hayupo, basi tutayafanya hata ikiwa ni Alhamisi wiki hii ilmuradi awe ofisini,” akasema Bw Omar.

Gen Z mwingine alisema katu hawatalegeza kamba katika kuisukuma serikali ya kitaifa na ile ya kaunti kutenda haki.

Alisema furaha yao ni kuona kuna uwazi na uwajibikaji katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Tunakataa ufisadi, ukabila na kila aina yoyote ya uovu serikalini. Twapigania matumizi ya fedha za umma yawe ya kisawa. Tutaandamana hadi pale vilio vyetu vyote vitakaposikika,” akasema kijana huyo.

Uchunguzi wa Taifa Leo ulibaini kuwa Bw Timamy alikuwa miongoni mwa magavana sita wa Pwani ambao juma lililopita walisafiri nchini Italia kutafuta fedha na wawekezaji katika sekta ya Uvuvi na Uchumi wa Baharini kwa jumla.

Licha ya magavana hao kurudi kutoka nje ya nchi, Bw Timamy bado hajaweza kuwasili au kuonekana Lamu tangu juma hili lianze.