Ubatizo wa pili wa Waziri Wandayi stima zikikatika kote nchini isipokuwa Bondeni
SEHEMU nyingi za Kenya hazina stima baada nguvu za umeme kukatika kote nchini kwa mara ya pili ndani ya wiki moja Ijumaa.
Kampuni ya kusambaza stima, Kenya Power, imetangaza kuwa stima zilikatika katika kaunti nyingi isipokuwa chache za Bonde la Ufa.
Kupitia ilani, kampuni ilisema kwamba stima zilikatika Ijumaa kuanzia saa tatu asubuhi isipokuwa Bonde la Ufa.
“Tunaomba radhi kwa tatizo hili. Tumekumbwa na ukosefu wa stima unaoathiri sehemu kadhaa za nchi. Tunajitahidi kutatua shida hii haraka iwezekanavyo,” kampuni ilisema.
Tukio hili linajiri saa chache baada ya Waziri wa Kawi na Mafuta ya Petroli Bw Opiyo kuhakikishIa Wakenya kuwa kukatika kwa stima kutatatuliwa.
Akizungumza alipozuru afisi za Kenya Power, Nairobi, Bw Wandayi alisema kuwa wizara ina mikakati ya kuzuia mtindo wa kukatika kwa stima kila mara.
“Nilichokuja hapa kusema ni kuwa tumeweka mikakati na mifumo ambayo itazuia kupotea kwa stima, lakini ikitokea kutakuwa na mfumo wa kurejesha stima haraka,” Bw Wandayi alisema Alhamisi.
Mnamo Ijumaa, Kenya Power ilisema itafahamisha Wakenya hatua itakazochukua kurudisha stima baada ya kukatika sehemu nyingi nchini.