Ubomoaji: Familia 300 zatafuta makazi mbadala
NA SAMMY KIMATU
FAMILIA zaidi ya 300 zimelazimika kuhama makwao baada ya serikali kubomoa nyumba zao katika eneo la Budalangi katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kayaba, tarafa ya South B kwenye kaunti ndogo ya Starehe.
Aidha, Naibu Kamishna katika kaunti ndogo ya Starehe, Bw John Kisang, aliambia wanahabari kwamba shughuli hiyo ilikuwa mojawapo ya zilizoratibiwa na serikali kufuatia agizo la Rais William Ruto kwamba nyumba, vibanda na majengo yote yaliyo katika mikondo ya maji kote nchini yabomolewe.
Bw Kisang alisema kando na nyumba zilizobomolewa, vibanda vya kuuzia bidhaa na chakula na vingine vya biashara ya vyuma chakavu pia zilibomolewa.
Aidha, aliongeza kwamba katika kampuni ya Glory Paints mkabala wa barabara ya Likoni, tingatinga lilibomoa ua na lango la kutumiwa wakati wa dharura akisema vyote vilivyobomolewa vilikuwa katika mkondo wa maji katika Mto Ngong.
Wakati mmoja, makumi ya vijana walishinda nguvu polisi na Vijana wa Huduma Kwa Taifa kuweza ulinzi katika uwanja mmoja wa mfanyabiashara wa Jua Kali mmoja unaotumiwa kama karakara ya kutengeneza rangi, stoo ya bidhaa za plastiki, vyuma, nyaya za stima, tanki na katoni miongoni mwa zingine.
Akiongea na Taifa Leo kwa njia ya kipekee, mmiliki wa biashara hiyo amabaye pia anamiliki msururu wa nyumba za kupanga, Bw Samuel Mutinda alisema mali ya zaidi ya Sh25M iliporwa na vijana huku nyingine ikiharibiwa na tingatinga.
“Nimepata hasara ya zaidi ya Sh25M baada ya bidhaa kuporwa na vijana huku polisi na vijana wa NYS wakitazama. Tingatinga pia iliponda nyumba zangu nyingi,” Bw Sammy akasema.
Akijibu kuhusu shutuma, lawama na tetesi kuhusu utepetevu za maafisa wake, Kamanda wa polisi kaunti ndogo ya Makadara, Bi Judith Nyongesa alisema polisi hawana taarifa rasmi katika rekodi za malalamishi kwenye kitabu cha matukio (OB).
“Nilipeana maafisa wa kutosha kulinda kampuni ya Glory Paints. Hatuna ripoti ya malalamishi kuhusu Bw Mutinda ambaye awali alikuwa ameonywa, kupewa notisi na kufahamishwa mapema na serikali kwamba anaendesha biashara katika eneo la mkondo wa maji katika Mto Ngong,” Bi Nyongesa akahoji.
Baada ya wapangaji na wamiliki wa nyumba karibu na eneo la tukio ikiswemo walio na makazi mtaani wa mabanda wa Mukuru-Maasai, Karanjo-Kayaba na Maasai Village, wenyeji walianza kubomoa nyumba zao huku akinamama wakiwa na watoto migongoni wakikusanya vyombo vya nyumba, vifaa vya kielektroniki na nguo.
Tukienda mitamboni, Bw Kisang alithibitisha kuwa mafuriko yanayoathiri wakazi mtaani wa Kayaba karibu na daraja la Hazina/Kayaba yamechangiwa na viongozi wa mitaa na maafisa wa utawala waliohudumu kitambo walioshirikiana kwa njia za kifisadi kufunika reli iliyoelekea katika Taasisi ya Mafunzo ya Reli (RTI).
“Baada ya kuuza ardhi katika kijiji kinachoitwa Mukuru-Matress, walimwaga mchanga juu ya reli na kisha kuanza kugawia mabwanyeye waliojenga nyumba za mabati na orofa za mawe huku wakibadilisha mkondo wa majai na kuyasukuma kuelekea upande wa Kayaba,” Bw Kisang akaambia Taifa Leo.
Kinachosumbiriwa ni kuona ikiwa serikali ya sasa itaangazia jinsi mkondo wa maji ulivyokuwa awali kabla ya wakaazi wanaoathirika Kayaba kusulubiwa kutokana na watu wachache waliojawa na tamaa ya kujaza matumbo yao.