• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
Ubomoaji Voi: Wakuu wa utawala wakataa kupokea simu

Ubomoaji Voi: Wakuu wa utawala wakataa kupokea simu

NA LUCY MKANYIKA 

VIONGOZI wa Kaunti ya Taita Taveta wakiongozwa na Gavana Andrew Mwadime, walipata muda mgumu kujaribu kusimamisha ubomoaji wa nyumba katika eneo la Msambweni mjini Voi mnamo Jumamosi, huku wakuu wa usalama wakikataa kupokea simu zao.

Gavana Mwadime na viongozi wengine waliwemo mbunge wa Voi Abdi Chome, walijaribu kuwasiliana na viongozi wa serikali ya kitaifa ili kuingilia kati na kusitisha ubomoaji huo, lakini juhudi zao ziligonga mwamba kwani hawakuchukua simu zao.

Bw Mwadime alisema kuwa alishangazwa na kuhuzunishwa na hatua ya serikali, ambayo aliita kuwa isiyo na ubinadamu na kinyume cha sheria.

“Nimejaribu kupiga simu kwa kila mtu niliyedhani angesaidia lakini hata wale maafisa wa serikali kuu wanaofanya kazi katika kaunti hii hawana haja na wenyeji. Hakuna yeyote anayepokea simu. Hili tukio limetughadhabisha kama viongozi,” alisema.

Gavana wa Taita Taveta Andrew Mwadime. PICHA | MAKTABA

Alisema kuwa walikuwa wameitisha mkutano na viongozi wa eneo hilo na jamii Jumamosi kujadili njia ya kusonga mbele lakini walishtushwa na yaliyotokea.

“Nataka watu wajue kuwa sisi kama viongozi wa eneo hili tumefanya juhudi zetu. Baadhi ya maafisa wa serikali ya kitaifa wamekataa kuchukua simu zetu,” alisema.

Alidai kuwa ubomoaji huo ulifanywa kinyume cha sheria na bila kutoa taarifa kwa wananchi wa eneo hilo.

“Nimepata taarifa Jumamosi asubuhi. Tumekuwa tukitafuta suluhu kwa muda. Tumeongea na idara tofauti lakini cha kushangaza polisi wamekuja na buldoza na kubomoa makaazi ya watu,” akasema.

Alisema kuwa serikali yake na viongozi wa eneo hilo walipendekeza kwa serikali ya kitaifa kununua ardhi hiyo kutoka kwa mwekezaji huyo ili kuwapa maskwota hao.

“Tulikuwa na pendekezo kuwa serikali ya kaunti na pia ya kitaifa itafute fedha ilipe mwekezaji ili tutatue shida hii. Tulikuwa pia tuna nia ya kutafuta ardhi mbadala ili watu wetu wasiondolewe,” akasema.

Mnamo Jumamosi, zaidi ya wakazi 3,500 walivamiwa na kikosi cha maafisa wa polisi waliokuwa wakiandamana na kikosi cha kubomoa nyumba ambacho kimebomoa nyumba kadhaa kwenye kipande cha ardhi inayozozaniwa.

Zaidi ya maskwota 3,500 katika kijiji cha Msambweni, Kaunti ya Taita Taveta wabaki bila makao baada ya kampuni ya Sparkle Properties Limited kuanza shughuli ya ubomoaji wa nyumba zao kwenye ardhi inayozozaniwa ya ukubwa wa ekari 90. PICHA | LUCY MKANYIKA

Ardhi hiyo inasemekana kumilikiwa na Sparkle Properties ambayo inadai kuinunua kutoka kwa kampuni ya viatu ya Bata.

Hata hivyo, wakazi wanasema kuwa wamekuwa wakiishi kwenye ardhi hiyo kwa miongo kadhaa baada ya Bata kushindwa kuendeleza ardhi hiyo kulingana na mkataba wa kupangisha.

Hata hivyo, duru za kuaminika zilisema kuwa kuwa Inspekta Jenerali Bw Japhet Koome ameagiza uchunguzi kuhusu ubomoaji huo.

Bw Koome amewaita Kamanda wa Polisi wa Pwani, Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Taita Taveta Patrick Okeri na kamanda wa polisi wa eneobunge Benastein Shari kwenye makao makuu kwa mahojiano.

  • Tags

You can share this post!

Ugavi wa pesa kwa mujibu wa idadi ya watu kuumiza Mlima...

Burudani: Waliovuma zama zao kuteseka hadi lini?

T L