Ubomoaji wa nyumba za maskwota 3,500 waanza Msambweni
NA LUCY MKANYIKA
ZAIDI ya maskwota 3,500 katika kijiji cha Msambweni kilichoko Voi katika Kaunti ya Taita Taveta wako katika hatari ya kubaki bila makao baada ya mwekezaji mmoja kuanza ubomoaji mnamo Jumamosi asubuhi.
Buldoza zilianza ubomoaji huo huku maskwota hao wakishuhudia nyumba zao zikiharibiwa na kuachwa bila makao.
Ubomoaji huo umesimamiwa na kikosi cha maafisa wa polisi wakiongozwa na Kamanda wa Kaunti hiyo Patrick Okeri.
Ni kufuatia amri ya mahakama iliyowaagiza maskwota hao kuondoka kwenye ardhi ya ukubwa wa ekari 90 ambayo inadaiwa kwamba mmiliki halisi ni kampuni ya Sparkle Properties Limited.
Mwekezaji wa ardhi hiyo ananuia kujenga jumba la maduka.
Anasema alinunua kipande hicho kutoka kwa kampuni ya viatu ya Bata.
Hata hivyo, maskwota hao wanadai kwamba wameishi kwenye ardhi hiyo tangu mwaka wa 1963 na hawajawahi kulipwa fidia na Bata au mwekezaji huyo.
Mgogoro wa ardhi umekuwa ukipiganiwa mahakamani kwa zaidi ya muongo mmoja, huku maskwota wakipoteza kesi zote.
Mnamo Machi 2023, Mahakama ya Rufaa iliidhinisha uamuzi wa Mahakama ya Mazingira na Ardhi ya Mombasa ambayo iliamuru kuwa mwekezaji huyo ndiye mmiliki halali wa ardhi hiyo na kuwaamuru maskwota hao kulipa Sh1 milioni kama fidia na gharama ya kesi.
Mnamo Jumamosi, viongozi wakiongozwa na Gavana wa Taita Taveta Andrew Mwadime na Mbunge wa Voi Abdi Chome walitembelea eneo hilo na kujaribu kusimamisha ubomoaji, lakini hawakufanikiwa.
Maskwota hao, ambao walikuwa walihuzunika na kukosa cha kufanya, walimwomba Rais William Ruto kuingilia kati na kuwaokoa kutokana na kufurushwa.
Walisema hawana mahali pengine pa kuenda na maisha yao yamesambaratika.
Wakazi walioathirika walimlaumu mwekezaji kwa kutumia mahakama kuchukua ardhi na pia wakalaumu serikali kwa kushindwa kuingilia kati na kuwalinda kutokana na kufurushwa.
“Hatupingi maendeleo, lakini tunapinga ukosefu wa haki. Mwekezaji angelifaa kutulipa fidia au kutupatia ardhi mbadala. Hatujui twende wapi,” alisema Bi Florence Wakio.
Alisema kufurushwa kwau kulikiuka haki zao za kibinadamu na akaitaka serikali kuwapa msaada wa kibinadamu ili waweze kuishi na familia zao.
“Serikali isiruhusu ukatili kama huu kufanyika kwa watu wake. Sisi ni Wakenya na tunastahili heshima na hadhi. Tumeachwa bila makao na maskini na hivyo tunaomba serikali iingilie kati na kutusaidia,” alisema.
Wito wa mazungumzo kati ya mwekezaji na wavamizi ili kupata suluhu ya amani kwa mgogoro wa ardhi iligonga mwamba.
“Wameharibu nyumba zetu na kutuacha bila makao. Tunateseka na tunahitaji msaada. Tunamuomba Rais asikie kilio chetu na kutuokoa kutokana na dhiki hii,” Bi Bahati Mwakio, mama wa watoto wanne, alisema.
Mkazi mwingine, Bw Shedrack Ominde alisema serikali ya Kenya Kwanza iliahidi kwamba ubomoaji hautafanyika wakati wa utawala wake na akaomba serikali kuingilia kati.
“Wakati wa kampeni zake, Rais alisema kuwa hakutakuwa na ubomoaji. Kinachotokea hapa leo hii ni kinyume na ahadi yake,” alisema Bw Ominde.
Katika mahojiano ya awali na Meneja Mkuu wa Sparkle anayesimamia mali za kampuni hiyo, Bw Francis Mulili, alisema wamefuata utaratibu unaofaa na kuthibitisha umiliki wa ardhi.
Alisema nia ya kampuni haikuwa kuwafurusha maskwota hao bali kujadiliana na wao kuhusu umiliki wa ardhi hiyo. Alisema juhudi zao ziligonga mwamba.
“Tumefuata sheria na kushinda kesi zote zikithibitisha umiliki wetu. Tumejaribu kuwashirikisha watu hao kwa amani, lakini wamekataa kushirikiana nasi. Hatuna budi ila kutumia sheria kurejesha mali yetu,” Bw Mulili alisema.