Uchimbaji dhahabu unavyotishia mazingira na kilimo
NA OSCAR KAKAI
KATIKATI mwa eneo la Tangasia na Tapach, chini ya milima na ndani ya msitu wa Marang’ar uvunaji dhahabu umeshika kasi.
Uchimbaji wa madini hayo yenye thamani huendelezwa majira ya usiku.
Wachumaji wengine, aidha, huchimba kisiri mchana ili kukwepa kukumbana na mkono wa sheria.
Ujanja huo, ni kwa sababu msitu huo ni raslimali ya serikali.
Pokot Magharibi, ni miongoni mwa maeneo machache nchini yaliyojaaliwa kuwa na dhahabu.
Hata hivyo, shughuli hiyo imegeuka kuwa mwiba mkali na kuathiri wakazi.
Maeneo ya nyanda za juu katika Kaunti Ndogo ya Pokot Kusini, hushuhudia maporomoko ya ardhi.
Malalamishi yameibuliwa kuhusu hange hiyo kuathiri mazingira, binadamu na hata wanyama.
Mwaka jana, 2023, mtu mmoja alipoteza maisha baada ya kufunikwa na migodi wakati akisaka dhahabu.
Licha ya kuwa wanasaka riziki, oparesheni hiyo ni hatari kwa maisha yao.
Wengi wa wachuma dhahabu wakilenga kutajirika upesi, uchunguzi unaonyesha eneo hilo kamwe si salama.
Mto wa Sukut, ulioko kati ya Lokesheni ya Tangasia na Kapsangar umeathirika pakubwa.
Isitoshe, machimbo hayo yanatajwa kuwa chocheo la wanafunzi kuacha masomo.
Baadhi ya wasichana wa shule wanaoshiriki zoezi la kuvuna dhahabu, wameishia kujipata kwenye ndoa za mapema.
Cha kushangaza zaidi, baadhi ya wenyeji wameasi shughuli za kilimo na kuingilia uchumaji dhahabu.
Miti, mito na vyanzo vya maji vimevamiwa na kuharibiwa.
Dennis Yarango’le, mkazi, anasema kuwa shughuli hiyo sasa inaelekezwa kwenye maboma ya watu hatua inayotishia kuwahamisha.
“Maji yameadimika kwa sababu ya mito kuvamiwa. Mashamba nayo, huenda hivi karibuni kilimo kikawa historia,” anaeleza.
Chifu wa Lokesheni ya Tangasia, Samuel Katumon anasikitikia mashamba kuharibiwa na vyanzo vya maji kuvamiwa.
“Ni hatari kwa maisha ya binadamu,” anasema.
Anasema kuwa mfumko wa bei ya dhahabu umechochea wakazi kuendelea kuharibu mazingira.
“Udongo umeharibika na kilimo kimeathirika,” anasema Chifu Katumon.
Emmanuel Ting’anur, mchuma dhahabu anakumbuka jinsi aliponea kusafirishwa jongomeo wakati migodi iliporomoka.
“Kwa sababu ya ardhi kuharibiwa, udongo umekuwa dhaifu,” anasema.
Wiki iliyopita, Naibu Kamishna Kaunti Ndogo Pokot Kusini, David Boen aliamuru kusitishwa mara moja kwa shughuli zote za kuchuma dhahabu kwenye msitu wa Marang’ar.
Alisema kuwa viongozi wamekerwa na athari za wakazi kuendelea kuchimba dhahabu.
“Tumesimamisha shughuli hiyo hadi wakati serikali itakapotoa mwelekeo,” anasema.
Anasema kuwa lengo la kusimamisha shughuli hiyo ni kuzuia ajali ambazo husababisha vifo na majeruhi kwenye migodi.
‘‘Tumegundua kuwa wachimba dhahabu wamechimba mashimo mengi sana ambayo yanaharibu mazingira,’’ anasema Bw Bowen.
Analalamikia shughuli hiyo kuchangia watoto wenye umri mdogo – chini ya miaka 18 kuacha shule.
Wachimba dhahabu wanaendelea kumiminika, ikizingatiwa kuwa eneo hilo lina changamoto za miundomsingi kama vile ukosefu wa vyoo.
Ni hatari kwa uchafuzi wa mazingira, mkurupuko wa maradhi ukinukia.
Afisa huyo wa kiutawala anahimiza wenyeji kurejelea kilimo na ufugaji.
Kamanda wa polisi, Kaunti Ndogo ya Pokot Kusini Said Shungi, anasema kuwa eneo la Tapach ni chemichemi ya maji akisisitiza kuwa polisi hawataruhusu uchimbaji dhahabu ambao unaendelea kuharibu vyanzo vya maji.
‘‘Shughuli kama hizo ambazo hazina idhini ya serikali hazitaruhusiwa,’’ akaonya OCPD Shungi.
Afisa msimamizi wa misitu tarafa ya Lelan, Gordon Anyiko anasema kuwa jamii imekubali kuziba mashimo ambayo yametokana na uchimbaji dhahabu ili kuzuia watu kupoteza maisha na hata kujeruhiwa.