Uhasama wa kisiasa kati ya Lenku na Ole Kina watokota
UHASAMA wa kisiasa unatokota kati ya Seneta wa Narok Ledama Ole Kina na viongozi wa Kaunti ya Kajiado kuhusu mkutano ambao umepangwa kufanyika eneo la Sajiloni, Wadi ya Dalalekutu, Kajiado ya Kati.
Mnamo Alhamisi, Machi 3, 2025 Bw Ole Kina atakuwa mwenyeji wa mkutano huo ambao sasa unapingwa vikali na Gavana Joseph Ole Lenku, Seneta Samuel Seki na baadhi ya madiwani ambao wanaegemea Kenya Kwanza na Azimio.
Bw Ole Kina ametaja mkutano huo kama unaolenga kuyainua makundi lakini wanasiasa wanaoupinga wamedai kutengwa na kutohusishwa kwenye maandalizi yake.
Gavana Lenku Jumatatu, Machi 31, 2025 alimkashifu Bw Ole Kina kama mwanasiasa ambaye analenga kugawanya Wamaasai kwa kutumia mkutano huo.
Wiki jana, Mwenyekiti wa Baraza la Jamii ya Wamaasai tawi la Kajiado Richard Oloitipitip alipinga mkutano huo akisema unaegemea ukoo na unalenga kugawanya jamii za eneo hilo.
“Ledama ni mwanasiasa wakala ambaye anatumiwa kupiga mnada kura za Kajiado kuelekea uchaguzi wa 2027. Inasikitisha anawapuuza viongozi waliochaguliwa na ni vyema amakinikie masuala ya Narok wala si Kajiado,” akasema Bw Oloitipitip.
“Tuna viongozi ambao walichaguliwa kutoka vyama tofauti. Kama kuna suala ambalo linahusu jamii, tunakuja pamoja na kushirikiana lakini huu mkutano wa Ledama ni wa kupanda mbegu za chuki,” akasema.
Mwekahazina wa baraza hilo la wazee Jude Ole Ncharo naye alisema jamii hiyo ilimuunga mkono kiongozi wa ODM Raila Odinga mnamo 2022 na tayari amewaingiza serikalini kupitia ushirikiano na Rais Ruto.
“Tuko kwa serikali na hatutaki wakala wa kisiasa kutupeleka kwenye utawala wa Rais Ruto,” akasema Mzee Ncharo.
Ijumaa wiki jana, vijana wa Kajiado wakiongozwa na mwenyekiti wao Elian Martine na Rais wao Wenger Saigilu walisema mkutano wa Bw Ole Kina ni uchokozi kwa uongozi wa Kajiado.
“Ledama anatumiwa na watu wanaotaka uongozi Kajiado na wanawatumia watu wa nje. Lazima tuambie Ikulu iwadhibiti maafisa wao wanaolenga kugawanya jamii ya Wamaasai Kajiado,” akasema Bw Martine.
Kumekuwa na madai kuwa afisa wa ngazi ya juu Ikulu analenga kiti kikubwa Kajiado lakini kwa kuwa anazuiwa kushiriki siasa, anamtumia Seneta Ole Kina kumwendeshea kampeni kali.
Licha ya pingamizi hizo, Bw Ole Kina amesisitiza kuwa mkutano wake utaendelea wala hahitaji ruhusa ya kuuandaa.
Mamia ya vijana nao wamesimama naye na kusema watahudhuria mkutano huo.
“Nina nyumba kadhaa Kajiado, mimi ni mkazi wa Kajiado na sihitaji ruhusa yao. Mkutano wangu utaendelea,” akasema.