Habari za Kaunti

Ujenzi wa bwawa na visima kupunguza mizozo

March 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA WINNIE ATIENO

SERIKALI imetenga kima cha Sh48 milioni zinazolenga kutumika kujenga vyanzo vya maji (water pan) na visima katika kaunti ya Tana River ili kupunguza masaibu ya wafugaji katika kaunti kutokana na kame.

Akizungumza katika kijiji cha Kone, Afisa Mkuu Mtendaji wa Mamlaka ya Kitaifa ya Kukabiliana na Ukame, Bw Hared Adan alisema visima hivyo pia vitasaidia wakazi katika eneo hilo na kaunti jirani za Wajir na Garissa.

Bw Adan alisema mradi huo utasaidia kupunguza migogoro ya maji wakati wa ukame.

Msimu wa ukame, mizozo ya rasilimali kwa kawaida huzuka kati ya binadamu na wafugaji kutokana na uhaba wa maji unaoshuhudiwa.

“Tunataka bwawa liwe na maji ambayo yatatumika na wenyeji na wenzao katika kaunti jirani. Lakini nawarai wakazi watumie maji vizuri. Mradi huu ni kwa manufaa yenu binafsi,” alisema Bw Adan.

Mwenyekiti wa mamlaka hiyo Bw Shallow Yahya alisema mradi huo utatumia teknolojia ya kawi ya jua.

Alisema mamlaka hayo itajenga mabwawa mengine ili kusaidia wafugaji kupata maji ya mifugo yao.

Tana River ni mojawapo ya kaunti zinazoorodheshwa kuwa kati ya maeneo jangwa na nusu jangwa nchini (Asal).