Habari za Kaunti

Ujumbe kutoka nchi ya Mfalme Mswati III wasisimua Murang’a

May 16th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA MWANGI MUIRURI

GAVANA wa Murang’a Bw Irungu Kang’ata amepokea ujumbe kutoka Eswatini uliofika kujifahamisha mengi kuhusu masuala ya ugatuzi. 

Ujumbe huo ulivutia wenyeji ambao husikia sifa za jinsi Mfalme Mswati III hujipa mrembo wa kuoa akipenda.

Kupenda huko hadi sasa kumemwacha akiwa na wake 15 na watoto 36.

Wenyeji wa Murang’a hawakuficha tamaa yao ya kuwaona wanawake waliokuwa katika ujumbe huo huku wengi wakikubali walikuwa wa kuvutia.

Ujumbe huo uliongozwa na Waziri wa Maendeleo ya Miji katika serikali ya Eswatini Apolo Mapalala na ambaye alikuwa amevalia mavazi mfano wa shuka kama yale yanayopendwa na jamii ya Maa nchini Kenya na Tanzania.

Ujumbe kutoka Eswatini ukiwa katika Kaunti ya Murang’a. PICHA | MWANGI MUIRURI

Ujumbe huo ulikuwa na nia ya kujifahamisha na jinsi ambavyo serikali za ugatuzi hufanya kazi nchini Kenya, Murang’a ikiteuliwa kupokea ujumbe huo.

Ujumbe huo ulitembezwa kujionea mafanikio ya miradi mbalimbali ya kaunti, ikiwemo ile ya kutumia teknolojia katika hospitali, kuwapa wakulima ruzuku na pia miradi kadha ya afya na elimu ya chekechea.

“Niko tayari kwa wakati wowote kupokea ujumbe kutoka taifa la Eswatini ili kuwanoa kuhusu utekelezaji miradi, ukiwemo ule wa kuwapa watoto wa shule uji,” akasema gavana Kang’ata.

Waziri Mapalala alisema amefurahishwa na urafiki na ushirikiano kati ya Kenya na taifa lake, ambalo zamani liliitwa Swaziland, akisema urafiki huo utaboreshwa zaidi katika siku za usoni.

Wengi wa waliofika kumpojea Mapalala na ujumbe wake walisema kwamba wangetaka kufika nchini Eswatini hasa wakati wa hafla ya Mfalme Mswati kujipa mke mwingine endapo hilo litatokea.

[email protected]