Ukame wasababisha uhaba wa chakula kaunti za Mlima Kenya
WAKATI wa msimu wa kawaida, Bw Gerald Murira, mkulima kutoka Ntumburi eneo la Buuri, Kaunti ya Meru, angekuwa akijiandaa kuvuna magunia 40 ya maharagwe.
Hata hivyo, msimu wa mavuno unapokaribia katika eneo hilo, Bw Murira na majirani zake wanaotegemea mvua kukuza mahindi na maharagwe wanakabiliwa na mashamba matupu.
“Mvua ilinyesha kwa kuchelewa na ndani ya wiki mbili tu, mazao yalinyauka. Tangu wakati huo tumesahau kabisa kuwa tulipanda. Ni wakulima waliokuwa na maji ya kunyunyuzia pekee ndio walioweza kuokoa mazao yao,” anasema Bw Murira.
Hali anayopitia Bw Murira ni sawa na ile ya wakulima katika maeneo mengi ya Meru, Tharaka Nithi, Embu, Nyeri, Kirinyaga na Murang’a ambako wakazi hutegemea mahindi na maharagwe kama chakula cha msingi.
Takwimu kutoka Wizara ya Kilimo zinaonyesha kuwa katika mwaka wa kawaida, kaunti hizi sita huzalisha zaidi ya tani 333,000 za mahindi na karibu tani 130,000 za maharagwe.
Hata hivyo, kufikia mapema Desemba, wakulima katika eneo hilo walianza kupata hasara baada ya mazao kunyauka kutokana na mvua duni.
Kulingana na Idara ya Hali ya Hewa nchini (KMD), vituo vingi kote nchini vilinakili kiwango cha mvua kilicho chini ya wastani kati ya Oktoba na Desemba, hali iliyoathiri pakubwa uzalishaji wa chakula.
“Mvua iliyo chini ya wastani ilisababisha ukosefu wa unyevu wa kutosha kwenye udongo, hali iliyozua mazingira yasiyofaa kwa ukuaji wa mimea na maendeleo ya mazao katika maeneo kadhaa ya nchi,” ilisema ripoti ya kila mwezi ya Desemba.
Mkurugenzi wa Hali ya Hewa Kaunti ya Meru, Justin Murithi, alisema sehemu kubwa ya kaunti hiyo ilipokea mvua chache, jambo lililosababisha mazao kukauka.
“Baadhi ya maeneo ya Igembe Kaskazini hayakupokea mvua yoyote. Kufikia mapema Desemba, mazao mengi yalikuwa yamekauka. Ni baadhi tu ya maeneo ya Imenti Kaskazini, Imenti Kati na Imenti Kusini yanayotarajiwa kupata asilimia 50 ya mavuno ya kawaida. Hivyo basi, hali ya utoshelevu wa chakula si nzuri. Tumeshauri serikali ya kaunti na ya kitaifa kuharakisha misaada,” alisema Bw Murithi.
Ripoti ya awali ya Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Ukame (NDMA) pia ilionyesha kuwa kukauka kwa mazao kulianza mapema katika kaunti za Kirinyaga, Murang’a na Nyeri.
Katika eneo bunge la Kieni, Nyeri, athari zimeanza kujitokeza huku bei za chakula zikiongezeka kwa kasi.
Katika soko la Chaka, debe la viazi lililokuwa likiuzwa kwa Sh400 sasa linauzwa Sh600, huku gunia la kilo 90 la mahindi likiuzwa kati ya Sh4,800 na Sh5,000, kutoka Sh3,000 wakati kama huu mwaka jana. Hali hii imewalazimu wafanyabiashara kutafuta bidhaa kutoka kaunti jirani.
Mwenyekiti wa soko hilo, Bi Jane Wangechi, anasema hali hiyo imechangiwa pakubwa na mvua kukosa kunyesha.
Eneo hilo hutegemea sana mvua na miradi ya maji ya kijamii kwa shughuli za kilimo.
“Mvua tuliyopata katika miezi iliyopita ilikuwa chache sana. Mwezi uliopita ilinyesha kwa wiki moja tu, na mvua hiyo ilikuwa kali mno kiasi cha kuharibu mazao mashambani. Baadaye jua kali likafuata. Chakula tulichonacho kitaisha hivi karibuni,” alisema.
Wafanyabiashara wamelazimika kuagiza nafaka na mboga kutoka Nyandarua, na Kirinyaga. Hata hivyo, juhudi hizi mara nyingi zimekuwa bure, huku baadhi ya malori yakirejea bila mzigo kutokana na uhaba wa chakula katika maeneo hayo pia.
Hali hii imesababisha serikali kuingilia kati kwa kusambaza chakula cha msaada. Hata hivyo, baadhi ya wakazi wanasema zoezi hilo halifanywi kwa haki.
Mkazi wa Naromoru, Bw Joseph Mwangi, alisema chakula cha msaada kinachotolewa na wanasiasa kimegeuzwa kuwa zana ya kampeni na mara chache huwafikia walio hatarini zaidi.
“Kimekuwa kama zawadi ya kisiasa kwa wale walio na uhusiano na maafisa wa serikali. Serikali inafaa kurejea kuwawezesha wakulima kwa kutoa mbolea na pembejeo za kilimo ili kuokoa hali,” alisema.
Aliongeza kuwa kuna haja ya kuwekeza katika suluhisho za muda mrefu, ikiwemo ujenzi wa mabwawa na upanuzi wa miradi ya maji ya kijamii.
Mkurugenzi wa Kilimo Kaunti ya Meru, Martin Munene, alisema hali hiyo inaleta changamoto kubwa ya utoshelevu wa chakula.
Kwa mujibu wa Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku, serikali iko tayari kukabiliana na uhaba wa chakula unaotokana na mvua kukosa.
Ripoti ya DAVID MUCHUI, MERCY MWENDE na GEORGE MUNENE