Ukatili: Mwanaharakati wa LGBTQ alinyongwa hadi kufa
NA TITUS OMINDE
MWANAPATHOLOJIA Mkuu wa Serikali, Dkt Johansen Oduor mnamo Jumanne, Aprili 9, 2024 aliambia Mahakama Muu mjini Eldoret kwamba mwanaharakati wa LGBTQ, Edwin Kiptoo almaarufu Chiloba alinyongwa hadi kufa.
Akitoa ushahidi wake mbele ya jaji Reuben Nyakundi, Dkt Oduor aliambia korti kuwa Bw Chiloba alikufa kwa kukosa hewa ya Oksijeni baada ya soksi tatu kujazwa mdomoni na kufungwa puani kwa kutumia suruali ndefu.
Jackton Odhiambo almaarufu Lizer ndiye mshukiwa mkuu wa mauaji hayo.
Mwanapatholojia huyo aliambia mahakama kwamba mwanafunzi huyo wa Chuo Kikuu cha Eldoret mwenye umri wa miaka 26 aliuawa kikatili.
Wakati wa uchunguzi wa maiti, Dkt Oduor alisema kuwa mwili wa Chiloba ulikuwa ukioza na kuanza kutoa harufu mbaya.
“Marehemu alikuwa amefungwa soksi tatu mdomoni na mguu mmoja wa suruali ya jeans ulikuwa umefungwa kwa nguvu mdomoni na puani. Alipata michipuko sehemu ya ndani ya midomo ya juu na ya chini na upande wa kushoto wa ulimi,” Dkt Oduor aliambia mahakama.
Alidokeza kuwa Chiloba hakuwa na majeraha yoyote nje.
Dkt Oduor alieleza mahakama kuwa baadhi ya sampuli kutoka kwa marehemu zilichukuliwa kwa uchunguzi zaidi na kuchunguzwa katika maabara ya serikali ili kuoanisha na sampuli zilizochukuliwa kutoka kwa mshtakiwa.
Koplo Mercy Kathure, Afisa wa Upelelezi katika kesi hiyo, alisimulia kupokea habari kuhusu sanduku la chuma lililokuwa limetupwa barabarani asubuhi ya Januari 3, 2023.
Alisema alielekea eneo la tukio na wenzake kukagua kisanduku hicho kwa vile mashahidi waliowapigia simu polisi walikuwa wameripoti kwamba dereva wa gari la Toyota aliyekuwa akiendesha kwa kasi alitupa sanduku hilo kwenye barabara ya Kipkenyo-Kaptinga Kapseret, Kaunti ya Uasin Gishu.
Mchunguzi huyo aliambia mahakama alipofungua sanduku hilo kubwa, walipata mwili wa marehemu uliokuwa ukioza ambao ulisafirishwa hadi katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi (MTRH) kuhifadhiwa kama mwili ambao haukuwa umetambuliwa.
Alisema kuwa baadaye alifahamu kupitia mitandao ya kijamii kuwa mwili huo ulikuwa wa mwanaharakati maarufu wa LGBTQ na mwanamitindo Edwin Kiprotich Kiptoo almaarufu Chiloba.
Dereva wa teksi ambaye alikuwa amekodisha gari la Toyota fielder kwa mshukiwa mkuu Jackton Odhiambo alikamatwa na watoto wawili waliokuwa wamemsaidia mshtakiwa kupakia sanduku kwenye gari hilo pia walikamatwa.
Bw Odhiambo alikanusha kumuua mwanamitindo huyo anayesemekana kuwa mpenzi wake katika kisa kilichotokea kati ya Desemba 31, 2022 na Januari 3, 2023 Noble Breeze Apartments katika eneo la Chebisaas, Kaunti Ndogo ya Moiben, Uasin Gishu.
Kesi hiyo itaendelea kusikizwa mnamo Mei 7.