Umoja utadumu? Jinsi uchaguzi Magarini ulifaulu kuleta mahasimu Joho, Kingi meza moja
UCHAGUZI mdogo wa Magarini uliweka kwenye mizani umoja wa viongozi wa kisiasa wa Pwani, ambao wamekuwa na mgawanyiko kwa miaka mingi.
Kwa muda mrefu, wanasiasa katika ukanda huo wamekuwa wakiegemea vyama tofauti vya kisiasa, hali ambayo husababisha ushindani wa ubabe.
Hata hivyo, uchaguzi mdogo ulifanikiwa kuwaleta pamoja wanasiasa wakiwemo Waziri wa Madini, Bw Hassan Joho, na Spika wa Seneti, Bw Amason Kingi, hali iliyochangia ushindi wa Bw Harrison Kombe katika wadhifa huo wa ubunge.
Akizungumza katika mojawapo ya mikutano wakati wa kampeni za uchaguzi huo, Bw Joho aliwahimiza wakazi kushirikiana na viongozi ambao wameungana serikalini kupitia ushirikiano wa Rais William Ruto na aliyekuwa kiongozi wa ODM Raila Odinga, almaarufu kama broad-based.
“Mimi, Kingi na hata Salim Mvurya (Waziri wa Michezo) tuko pamoja kwa hivyo tushirikiane sote ili tutimize malengo yetu ya Pwani,” alisema Bw Joho.
Watatu hao, ambao ni magavana wa zamani wa Mombasa, Kilifi na Kwale mtawalia, waliwahi kushirikiana pamoja katika ODM.
Hata hivyo, ushindani wa ubabe wa kisiasa ulisababisha Bw Mvurya kuondoka chamani humo akawania kipindi cha pili cha ugavana kupitia Chama cha Jubilee mwaka wa 2017.
Baadaye aliungana na Rais Ruto katika Chama cha UDA.
Kwa upande mwingine, Bw Kingi alianzisha chama chake cha Pamoja African Alliance (PAA) muda mfupi kuelekea kwa Uchaguzi Mkuu wa 2022 katika juhudi zake za kushinikiza Pwani kuungana chini ya chama kimoja cha ukanda huo.
Viongozi wa upinzani wanahoji kuwa, ushirikiano ulioonekana wakati wa uchaguzi mdogo ulichangiwa pakubwa na maelewano ya ‘broad-based’, ambayo hatima yake ifikapo mwaka wa 2027 bado haiko wazi.
“Ifikapo 2027 hakutakuwa na kitu kama ‘broad-based’. Hawa rafiki zangu wote watakuwa na misimamo mingine tofauti,” kiongozi wa Chama cha Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, alisema katika mojawapo ya mikutano ya kisiasa Magarini. Bw Musyoka ndiye aliongoza kampeni za mgombea wa Chama cha DCP, Bw Stanley Kenga, ambaye aliibuka wa pili katika uchaguzi huo.
Mnamo Jumatano, Gavana wa Kilifi, Bw Gideon Mung’aro, aliandamana na Bw Kombe kwa mkutano na Rais Ruto katika ikulu ya Nairobi.
Bw Mung’aro alisema mkutano huo ulikuwa wa kujadili mipango kuhusu utekelezaji wa ahadi zilizotolewa wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo.
Miongoni mwa miradi iliyotajwa wakati wa kampeni ni ujenzi wa barabara ya Mjanaheri–Ng’omeni, ambayo gavana alisema ukitekelezwa utaleta mabadiliko makubwa.