Habari za Kaunti

Utulivu warejea Kibiko baada ghasia kuhusu ardhi inayozozaniwa

Na STANLEY NGOTHO January 3rd, 2026 Kusoma ni dakika: 2

HALI ya kawaida imerejea katika ardhi tata ya Kibiko huko Ngong, Kaunti Ndogo ya Kajiado Magharibi, baada ya wiki mbili za ghasia zilizosababisha kifo cha afisa mmoja wa polisi, raia kujeruhiwa na mali kuharibiwa.

Kwa muda wa wiki mbili, hali ya taharuki imekuwa ikitanda kufuatia zoezi la kuweka mipaka choni ya ulinzi wa polisi katika shamba hilo lenye ukubwa wa ekari 2,800 na thamani ya Sh100 bilioni linalodaiwa na sehemu ya wanachama 16,000 wa Keekonyokie Community Land Trust.

Vijana waliokuwa wamejihami kwa silaha walikuwa wakizunguka eneo hilo tete, hali iliyochochea hofu, mvutano na ghasia.

Hata hivyo, Ijumaa, siku mbili baada ya kikosi cha maafisa wa polisi wa kawaida na wa GSU kuondoka eneo hilo kufuatia kukamilika kwa zoezi la kugawa ardhi, utulivu umerejea. Wakazi wa maeneo yanayopakana na Kaunti ya Kiambu wameanza tena shughuli zao za kila siku.

Hata hivyo, wanawake kadhaa walioumia kutokana na risasi za mpira bado wanapokea matibabu huku vijana wanne waliokamatwa wakati wa ghasia hizo wakiendelea kuzuiliwa na polisi.

Bi Agnes Kirer, 37, aliyepigwa risasi ya mpira begani, alikuwa akipata nafuu nyumbani kwake. Mama huyo mjane wa watoto saba alisema amelala kitandani kwa wiki moja sasa tangu alipotoka hospitalini.

“Nilijikuta katikati ya vurugu. Sasa ninategemea msaada wa watu wenye mapenzi mema kunisaidia mimi na watoto wangu. Ni serikali gani inayoshambulia wanawake na watoto kwa sababu ya ardhi?” alihoji.

Mzee Tauta Kamuasi, 70, alisema utulivu wa sasa ulitokana na kuondoka kwa polisi katika ardhi hiyo.

“Uwepo mkubwa wa polisi ndio ulikuwa kichocheo cha ghasia. Watu wenye nguvu wanatumia polisi kututisha kwa sababu wanatamani ardhi yetu. Hatutanyamazishwa,” alisema Bw Tauta ambaye ameishi katika eneo hilo kwa miaka 25.

Wanachama waliokata tamaa wanaamini kuwa chanzo cha ghasia hizo ni fidia inayosubiriwa ya bomba la mafuta linalopita katika ardhi hiyo yenye rutuba pamoja na watu kutoka nje wanaolenga kunyakua ardhi hiyo.

Bw Julius Lemoi alisema kitovu cha ghasia hizo ni fidia ya Sh2.4 bilioni kutokana na bomba la Kenya Pipeline Company (KPC). Bomba hilo linachukua takribani ekari 27.

Miaka michache iliyopita, kundi moja la uongozi wa Keekonyokie Community Land Trust liliwasilisha ombi kwa KPC kupitia Wizara ya Nishati na Petroli na Hazina ya Kitaifa kusitisha fidia hiyo hadi masuala muhimu yatatuliwe.

“Baadhi ya mabroka wa Nairobi wakishirikiana na watu fisadi katika Wizara ya Ardhi wanasababisha ghasia hizi kwa lengo la kujipatia fidia ya bomba. Huu ni mpango uliopangwa vyema wa kuwatisha wanachama kwa nia fiche. Wachukue fidia lakini waache ardhi yetu,” alisema Bw Lemoi.

Waziri wa Kaunti anayesimamia Ardhi, Hamilton Parseina, alisema hatimiliki hizo hatimaye zitafutwa akisema mchakato huo ulikuwa wa ulaghai.

“Mwishowe hatimiliki hizo zitakuwa batili. Zitafutwa na taasisi husika ukweli utakapobainika. Hatutalegeza msimamo wetu kama kaunti katika kupigania haki ya watu wetu wa Keekonyokie,” alisema Bw Parseina.

Bw Topua Lesinko, wakili wa Mahakama Kuu anayewakilisha kundi la wanachama wanaopinga ugawaji uliokamilika, alisema uamuzi wa kesi ilyowasilishwa katika Mahakama ya Rufaa Nairobi dhidi ya ugawaji huo umepangwa kutolewa Januari 30, 2026.

“Tunasubiri uamuzi muhimu wa kesi iliyo mbele ya jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa Nairobi Januari 30 2026. Tuna matumaini kuwa mahakama itatoa uamuzi na wale watakaopatikana na hatia ya kudharau mahakama wataadhibiwa,” alisema Bw Topua.

Kiini cha mgogoro huo ni ugawaji wa shamba hilo la thamani la ekari 2,862 lililoko pembezoni mwa mji wa Ngong.

Ardhi hiyo ilirejeshwa kwa jamii na serikali baada ya kufungwa kwa mipango ya ufugaji wa mifugo mwanzoni mwa miaka ya 1980.

Makundi mawili hasimu yamekuwa yakikabiliana katika mvutano wa uongozi kwa zaidi ya miaka 10, hali iliyowagawanya wanachama. Kundi moja linaongozwa na mwenyekiti wa muda mrefu Moses Parantai huku kundi lililojitenga na kutekeleza zoezi la kuigawa likiongozwa na Bw Moses Monik.