Uvundo wafukuza wateja wa bidhaa jijini
FRIDAH OKACHI Na WINNIE ONYANDO
WATEJA wa bidhaa mtaani Kawangware, Nairobi wameanza kuhepa masoko yenye uvundo huku wauzaji wakiomba serikali ya kaunti kusafisha maeneo hayo.
Wakazi wa Kawangware nao wanaitaka serikali ya kaunti kufunga madampo kadhaa kutokana na afya zao kuathirika.
Nazo barabara katika maeneo hayo zimeharibika.
Kilomita nane kutoka katikati mwa mji la Nairobi tunakutana na wakazi wa Kawangware na wafanyabiashara wanaosema harufu mbovu imeongezeka kutoka kwa taka wakati huu wa mvua.
Katika kituo cha matatu cha Congo, harufu ya uvondo huo ndio inakukaribisha unapoingia mtaa huo.
Wachuuzi wa chakula wameibua wasiwasi juu ya hatari inayokabili biashara zao kutokana na uchafuzi huo.
Pia, wanahofia chakula huenda kikachafuliwa na uchafu ambao unaweza kusababisha kipindupindu. Kulingana na Bi Anne Kemunto, wanapoteza wateja kwa ambao wametoroshwa na harufu mbaya.
“Nilikuwa na biashara ya hoteli ambayo nilifunga mwezi Machi kwa sababu wateja wote walitoroka. Mteja alikuwa akiingia na wakati harufu inapomzidia pua kama sijampakulia chakula, anaondoka. Chakula kingi kilikuwa kikibaki na nikapata hasara kubwa,” alieleza Bi Kemunto.
“Wasimamizi wa afya ya umma na usafi wa mazingira wanapaswa pia kusaidia kutatua suala hili hapa. Kwa sababu jamii haiko salama tena na biashara zetu sasa ziko hatarini,” aliongeza Bi Kemunto.
Mfanyabiashara John Kamau aliambia Taifa Leo, kumekuwepo na ucheleweshwaji wa kukusanya taka hizo ambazo zimesambaa kando ya barabara ya Gitanga kabla ya eneo la Mlango Soko kwa muda wa miezi minne na kufanya eneo hilo kudharauliwa.
“Tumechoshwa na taka hizi zinazooza hapa. Tunashangaa kinachoendelea na mamlaka ya kukusanya taka au sisi si walipa ushuru kama Wakenya wengine kutendewa hivi?” aliuliza Bw Gateri.
“Siku hizi hatuwezi kula kwa amani ndani ya nyumba zetu kwa sababu ya uvundo unaokuja moja kwa moja kwenye vyumba vyetu vya kuishi. Hakuna hewa safi hapa,” aliongeza.
Mkazi wa eneo hilo, Bi Dorine Wanja, mama wa watoto watatu aliasema watoto wao wamekuwa wakipenda kucheza na kuokota vitu karibu na kituo hico cha taka kwa mikono, na hivyo kuwaweka kwenye hatari za kiafya.
“Utakuta watoto wakinunua ice creams kwa mikono ile ile ambayo haijanawa,” alisema Wanja.
Kutokana na mvua inayoendelea, maji yanayobeba taka hizo yanazidi kuzangaa kwenye barabara ya Gitanga huku barabara hiyo ikiharibika mbali na hatari ya kuleta maradhi.
“Taka hizi zimesonga hadi kwenye barabara. Magari yanasababisha msongamano kwa kuwa barabara imekuwa ndogo sana,” alieleza Bi Wanja.
Wakati huo huo, wakazi wa Nairobi wametahadharishwa dhidi ya kula vyakula vinavyochuuzwa msimu huu wa mvua ya mafuriko.
Mwenyekiti wa Kamati ya Afya katika bunge la Kaunti ya Nairobi, Maurice Ochieng, ametoa wito kwa wakazi wa Nairobi kuepuka kula vyakula vinavyochuuzwa ili kuepuka kuambukizwa magonjwa yanayosababishwa na mafuriko.
Akizungumza na wanahabai Jumanne, Bw Ochieng’ ambaye pia ni diwani wa wadi wa Mountain View alisema kwamba visa vya watu kuchuuza vyakula hasa katikati mwa jiji vimeongezeka, jambo ambalo anasema ni hatari kwa afya ya wakazi.
Aliwata wakazi kuepuka kula vyakula hivyo hasa wakati huu ambapo magonjwa yanayosababishwa na maji huenda yakaongezeka kutokana na mafuriko.
“Tumegundua kuwa watu wengi sasa wanachuuza vyakula kama vile ugali, mtura na kadhalika katikati mwa jiji. Hata hivyo, tunawatahadharisha wakazi kuepuka kula vyakula kama hivyo. Hii ni kwa sababu hujui wachuuzi hao wanatumia maji aina gani kuunda vyakula hivyo,” akasema Bw Ochieng.
Haya yanajiri huku mvua kubwa ikiendelea kuleta madhara katika maeneo mbalimbali.
Mvua imefanya majitaka kutapakaa kila mahali huku mitaro ikibaki wazi, jambo ambalo linaweza kusababisha ugonjwa wa kolera.
Mtiririko wa majitaka pia unafululiza katika baadhi ya makazi ya watu msimu huu wa mvua.