Viongozi wa Kajiado, wazee wapinga mkutano wa seneta wa Narok
Mvutano mkubwa umeibuka Kajiado kuhusu mkutano wa kisiasa unaopangwa na Seneta wa Narok, Ledama Ole Kina, kinyume na matakwa ya viongozi wa Kajiado.
Mkutano huo, unaotarajiwa kufanyika Alhamisi katika kijiji cha Sajiloni, Dalalekutuk, umepingwa vikali na Gavana Joseph Ole Lenku, Seneta Samuel Seki, na madiwani wa vyama vya UDA na Azimio.
Ingawa Ledama anadai kuwa mkutano huo ni wa kuwawezesha wanajamii, viongozi wa Kajiado wanaona kuwa una ajenda fiche. Gavana Lenku, katika hotuba ya hadhara, alimtaja Ledama kama mtu asiye na kazi maalum anayehusika na siasa za mgawanyiko. Baraza la Wazee wa Kimasai, likiongozwa na mwenyekiti Richard Oloitipitip, lilipinga mkutano huo, likisema kuwa unalenga kugawanya jamii kwa misingi ya kikabila.
“Ledama ni dalali wa kisiasa anayelenga kushawishi siasa za Kajiado kuelekea uchaguzi wa 2027. Ni aibu hajawashirikisha viongozi wa kaunti. Anapaswa kujishughulisha na masuala ya Narok,” alisema Oloitipitip.
Jude Ole Ncharo, mhasibu wa baraza hilo, alisema kuwa jamii ya Kimasai tayari ipo serikalini kupitia ushirikiano jumuishi wa kisiasa. “Hatuhitaji dalali wa kisiasa kudai kutupeleka kwa Rais Ruto,” alisema kwa hasira.
Vijana wa Kajiado, wakiongozwa na Elian Martine na Shadrach Wenger Saigilu, pia walipinga mkutano huo wakisema ni dharau kwa uongozi wa Kajiado. “Ledama anaungwa mkono na watu wa nje wanaotaka kuchukua uongozi wa Kajiado. Tunapaswa kuiambia Ikulu kudhibiti maafisa wake dhidi ya kugawanya jamii ya Kimasai,” alisema Martine.
Kwa upande wake, Ledama ameendelea na maandalizi kwa kununua mafahali kadhaa kutoka soko la Ilbissil ili kusaidia vikundi vya ufugaji. Pia, ametuma matingatinga kujenga barabara ya kuingia kijiji cha Eiti, ambapo mkutano utafanyika.
Akiwapuuza wakosoaji wake, Ledama alisema hahitaji ruhusa kufanya mkutano Kajiado. “Nina makazi Kajiado, sihitaji ruhusa kufanya mkutano hapa. Siasa za kibinafsi zimeathiri watu wetu kwa muda mrefu,” alisema.
Hali ya wasiwasi imeongezeka huku mamia ya vijana wasioalikwa wakiahidi kuhudhuria mkutano huo. Wadau wa siasa wanahofia kuwa huenda ghasia zikazuka ikiwa suluhu haitapatikana haraka.
.