• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 8:50 AM
Viongozi wa kidini Laikipia walalamikia ujangili, kuzorota kwa usalama

Viongozi wa kidini Laikipia walalamikia ujangili, kuzorota kwa usalama

NA MWANGI NDIRANGU

VIONGOZI wa Kanisa kutoka Kaunti ya Laikipia wamelalamikia ukosefu wa usalama eneo hilo huku wakitaka polisi na vitengo vingine vya usalama kuhakikisha kuna amani ya kudumu.

Mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la Makanisa Nchini (NCCK) ukanda wa Kati Susan Mugendi jana aliwaongoza kulalamikia kupanda kwa visa vya wizi wa mifugo hasa Kaunti ndogo ya Laikipia Kaskazini.

Bi Mugendi alisema majangili wamekuwa wakiwaua raia na kuwajeruhi Laikipia Kaskazini huku vitengo vya usalama wakilemewa kuzuia visa hivyo.

“Watu wameishi kwa hofu kwa siku nyingi na hili ni jambo ambalo halikubaliki kamwe. Majangili wamekuwa wakiwaua watu na kuharibu mali yao,” akasema Bi Mugendi.

“Pia tunakashifu kisa cha juzi ambapo polisi wa akiba aliuawa na watu wengine kujeruhiwa vibaya,” akaongeza kwenye mkutano na wanahabari mjini Nyanyuki.

Bi Mugendi akiwa ameandamana na maafisa wengine walisikitika kuwa serikali ya kaunti na ile ya kitaifa, zimekuwa zikitoa ahadi ya kumaliza ujangili lakini hilo halijafanikiwa.

Wakati NCCK ilipokuwa ikiwahutubia wanahabari, wakazi wa Lokesheni ya Ethi huko Laikipia Kaskazini waliandaa maandamano hadi afisi ya Kamishna wa kaunti mjini Nanyuki.

Wakazi hao walilalamikia utepetevu katika kupambana na ujangili na wizi wa mifugo.

  • Tags

You can share this post!

Kifo cha Kendereni: Kindiki asema polisi hawakumuua...

Vituko na vurumai katika mazishi ya Brian Chira

T L