Habari za Kaunti

Viongozi wadai kanuni zinakiukwa katika uchimbaji madini kijiji cha Kishushe, Taita-Taveta

Na KNA December 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

VIONGOZI wa Kishushe Ranching Cooperative Society Ltd wanaitaka Wizara ya Madini ifafanue taratibu za ridhaa ambazo serikali imeweka kwa wawekezaji wa madini wanaotaka kufanya shughuli zao ndani ya ardhi ya kampuni hiyo katika Kaunti ya Taita Taveta.

Katika kikao na waandishi wa habari mjini Voi, Katibu wa chama hicho, Bw Wilfred Mwalimo, alieleza wasiwasi kuwa ukiukaji wa taratibu katika utoaji wa leseni za uchimbaji kwa wawekezaji wanane ambao, kwa mujibu wa chama hicho, hawakupata ruhusa ya wanachama kama inavyotakiwa kisheria.

Kulingana naye, Sheria ya Madini ya 2016, inawataka wawekezaji kupata ruhusa ya wazi, ya mapema na iliyoandikwa kutoka kwa wamiliki wa ardhi kabla ya kuanza shughuli za uchimbaji.

Chama hicho kinasisitiza kuwa, hitaji hili la kisheria ni muhimu kulinda haki za ardhi za jamii na kuhakikisha ushirikiano wenye uwazi.

Mwenyekiti wa chama hicho, Bi Matilda Waleghwa, alisema kuna wawekezaji wawili pekee ambao walifuata taratibu ipasavyo, wakapata ruhusa ya wanachama kupitia Mikutano Maalum ya Wanachama (SGMs) kabla ya kuanza shughuli zao.

Bi Mwalimo alisisitiza kuwa, msimamo wa chama hicho si kupinga uwekezaji, bali ni kuhakikisha taratibu za kisheria zinafuatwa.

Mwenyekiti wa kamati ya usimamizi wa chama, Bw Mwashinga Mjomba, alisema tayari wamezungumza na wawakilishi wa wawekezaji mbalimbali na kuwahimiza kufuata taratibu sahihi kwa kuwasilisha mapendekezo yao katika mikutano ya wanachama.

“Tunataka wawekezaji waelewe kuwa sisi ndio wamiliki wa ardhi ya Kishushe na tunachotaka ni kuheshimiwa kwa haki zetu kupitia taratibu halali. Tunakaribisha uwekezaji lakini lazima ufanywe ipasavyo,” alisema.