Wachimba dhahabu 12 wakwama katika mgodi ulioporomoka
WACHIMBA dhahabu 12 wamekwama ndani ya mgodi uliporomoka katika kijiji cha Museno, Shinyalu, kaunti ya Kakamega Jumatano jioni.
Katika mkasa huo wa Jumatatu jioni, watu 20 wanasemekana kuwa ndani ya mgodi huo ambapo wanane waliokolewa wakiwa hai.
Mkuu wa polisi eneo kaunti ndogo ya Shinyalu Daniel Makumbu alisema shughuli za uokoaji zinaendelea kuwapata watu 12 ambao bado wamekwama katika mgodi huo.
“Tunaomba watu kuwa watulivu na waangalifu tunapoendelea na shughuli za uokoaji. Eneo karibu na mgodi ni hatari na tunaomba waepuke kukusanyika hapo kuepuka madhara zaidi,” alisema.
Kulingana na Bw Patrick Mukhule, mwenyekiti wa timu ya uokoaji eneo la Magharibi watu waliookolewa hawakuwa na majeraha lakini walikimbizwa hospitalini kwa uchunguzi wa kimatibabu.
“Mkasa ulitokea saa kumi na mbili jioni na shughuli za uokoaji zilianza mara moja,” alisema.
Mbunge wa Shinyalu Fredrick Lusuli alisema wale waliookolewa walikimbizwa hospitalini.
Visa vya migodi kuporomoka na kufunika wachimbaji madini sio geni katika kaunti ya Kakamega na maeneo mengine nchini.