• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Wachimbaji madini wapewa mafunzo kuepuka vifo migodini

Wachimbaji madini wapewa mafunzo kuepuka vifo migodini

NA LUCY MKANYIKA

SEKTA ya uchimbaji madini katika eneo la Taita Taveta inakabiliwa na hatari, huku visa vya ajali mbaya katika mashimo ya uchimbaji madini vikiendelea kuripotiwa katika eneo hilo.

Ili kuhakikisha usalama wa wachimbaji wadogowadogo katika eneo la uchimbaji madini, serikali na mashirika mbalimbali yameendelea kuwahimiza wachimbaji kufwata sheria na kudumisha usalama wanapoendesha shughuli zao.

Kaunti ya Taita Taveta ina utajiri mkubwa wa madini, haswa vito kama Tsavorites, ruby, garnet, na tourmaline miongoni mwa vingine.

Hata hivyo, katika miezi miwili iliyopita, wachimbaji wanne wamefariki katika matukio tofauti katika eneo la Mwatate.

Mnamo Novemba 2023, wachimbaji watatu waliaga dunia baada ya shimo lao kujaa maji ya mafuriko katika eneo la Kamtonga.

Nayo wiki jana, mchimbaji mwingine alipoteza maisha na wengine wanne kujeruhiwa baada ya shimo lao kuporomoka katika eneo la uchimbaji linalomilikiwa na Shirika la Madini ya Chawia, Mkuki.

Matukio yote yamehusishwa na ukosefu wa hatua na vifaa sahihi vya usalama.

Ili kupunguza visa hivi, Chama cha Wanawake katika Nishati na Uchimbaji nchini Kenya (Aweik) kimefanya mafunzo ya usalama na afya kwa wachimbaji wa eneo hilo.

Mafunzo hayo yalijumuisha utambuzi wa hatari, tathmini ya hatari, kushughulikia dharura, vifaa vya kinga, na afya kazini.

Baadhi ya maeneo ya uchimbaji yaliyotembelewa wakati wa mafunzo hayo ilibainika kuwa baadhi ya mashimo ya uchimbaji madini ya vito yalikuwa hatarini kuporomoka kwani hayakuwa yamethibitiwa.

Mengine yalikuwa hatarini kujaa maji wakati wa msimu wa mvua kwa sababu ya ukosefu wa njia za maji. Aidha, mashimo hayo hayana ngazi sahihi kwa wachimbaji kushuka na kutoka kwa urahisi.

Wachimbaji pia hawana vifaa sahihi vya kijikinga wakati wa shughuli zao za uchimbaji madini.

Mmoja wa wakufunzi, Mhandisi Peter Munyi, aliwaambia wachimbaji kuwa wanapaswa kufuata mwongozo na kanuni za usalama wakati wa kufanya kazi katika migodi ili kuepuka kuporomoka kwa mashimo yao na hivyo kuhatarisha kuzikwa hai.

Aliwashauri pia kuunda sheria ambazo zingewaongoza katika maeneo ya uchimbaji madini na kutafuta usaidizi kutoka kwa mamlaka husika.

“Lengo letu ni kuona wachimbaji wanapata thamani kwa shughuli zao na maisha yao yanalindwa,” alisema.

Mhandisi mwingine, Edwin Mwasi, aliwahimiza wachimbaji kuthamini maisha yao kwa sababu yalikuwa ya thamani zaidi kuliko madini waliyokuwa wakichimba.

“Hakuna haja ya kupoteza maisha yako wakati unatafuta vito. Unapoona maisha yako yako hatarini toka kwenye shimo ukiwa hai,” aliwaambia wachimbaji.

Alisema ikiwa wachimbaji watashindwa kutekeleza hatua zinazohitajika za afya na usalama inaweza kuwasababishia hasara.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Aweik Hannah Wang’ombe alisema ni jambo la kusikitisha kwamba wachimbaji walifariki kwa sababu zinazoweza kuzuilika.

Alisema kuwa Aweik ilijitolea kuwawezesha wachimbaji, haswa wanawake, kuboresha maisha yao na pia aliwahimiza wachimbaji kudumisha usalama na afya yao wakati wote.

“Unapaswa kuweka usalama wetu kwanza. Tutumie mafunzo haya na tujikumbushe mara kwa mara kuwa usalama wetu ni muhimu,” alisema.

Bi Wang’ombe pia aliwahimiza wachimbaji hao kuunda benki za vijiji kuweka pesa na pia kuchukua mikopo kupitia mpango huo.

Baadhi ya wachimbaji waliohudhuria mafunzo katika eneo la uchimbaji madini la Chawia CBO walibaini kuwa wanakabiliwa na changamoto kama vile ukosefu wa vifaa sahihi vya uchimbaji madini, fedha za kutekeleza hatua mbalimbali za usalama, na ukosefu wa masoko ya mawe yao.

Mjumbe wa bodi ya Chawia CBO Tom Mwashumbe alisema hatua za kuboresha usalama wao ni muhimu lakini alibaini kuwa wachimbaji wengi hawana uwezo wa kifedha kuzitekeleza.

“Tutaona cha kufanya kwa sababu tunajua umuhimu wa kulinda maisha yetu wakati tunatafuta madini haya,” alisema.

Mchimbaji mwingine Abdi Mohammed aliomba msaada zaidi kutoka kwa serikali na wadau wengine.

“Tunakabiliwa na changamoto nyingi hapa na ndio sababu hatuna uwezo wa kutekeleza hatua hizi,” alisema Bw Mohammed.

  • Tags

You can share this post!

Arsenal wasambaratisha kasri la Crystal kwa...

Afcon: Senegal wakomoa Cameroon na kutinga hatua ya 16-bora

T L