Habari za Kaunti

Viongozi wadai hakuna mkataba wa ‘kumi yako, kumi yangu’ baina ya jamii mbili Busia

Na TOBBIE WEKESA February 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

BAADHI ya viongozi kutoka kaunti ya Busia wamekana kuwepo kwa mkataba wowote kati ya jamii za kaunti hiyo kuhusu kiti cha ugavana.

Akihutubia waombolezaji katika mazishi ya Mzee Richard Maruti, 88, babake mwakilishi wadi ya Angurai Kaskazini Bw Isaac Wamalwa, Peter Imwatok ambaye pia ni kiongozi wa wengi katika Bunge la Kaunti ya Nairobi alifichua kwamba hakuna mkataba wowote uliowekwa baina ya jamii mbili kubwa katika kaunti hiyo.

“Wakati wa mazungumzo yaliyofanyika Bomas 2011, hakukuwa na mkataba wowote uliotiwa sahihi na jamii kuhusiana na ugavana wa Busia. Propaganda tunayoona ikienezwa na wenzetu ni uwongo. Mkataba uliowekwa unahusu utoaji wa huduma kwa wakazi wote wa kaunti hii,” alisema Imwatok.

Peter Imwatok akihutubia waombolezaji katika mazishi ya Mzee Richard Maruti, babake Mwakilishi wodi ya Angurai Kaskazini, Isaac Wamalwa. Picha|Tobbie Wekesa

Kauli ya Imwatok iliungwa mkono na aliyekuwa gavana wa kaunti hiyo Sospeter Ojamong aliyesema kwamba wakazi wa Kaunti ya Busia wana haki ya kumchagua yeyote kuwa gavana wao bila kushurutishwa na yeyote kufuata mkataba.

Ojamong alisema kwamba gavana atachaguliwa kulingana na utendakazi wake.

Katika hafla nyingine, spika wa Bunge la Kaunti ya Busia Bw Fredrick Odilo alisisitiza kwamba mkataba upo na unafaa kuheshimiwa.

“Kulikuwa na miaka kumi chini ya uongozi wa Sospeter Ojamong. Mheshimiwa Otuoma anamaliza miaka mitano kisha apewe mingine mitano ili akamilishe yake kumi kulingana na mkataba,” Odilo alisema.

Duru zinaarifu kwamba kinyang’anyiro cha ugavana katika kaunti ya Busia kinatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa baada ya Arthur Amugu Osiya, katibu katika ofisi ya Rais Ruto kutangaza azima yake ya kuwania kiti hicho.

Kwa sasa, Bw Osiya amezidisha kampeini zake huku akipuuza mazungumzo ya kuheshimu mkataba.