Wafanyabiashara walia kuumizwa na ushuru, ukatili wa kanjo
NA MWANGI MUIRURI
MBUNGE wa Kiharu Ndindi Nyoro amekiri kwamba Mamlaka ya Ushuru Nchini (KRA) na ile ya kupambana na bidhaa feki (CA) zinahangaisha wafanyabiashara nchini.
Akihutubia katika hafla ya maombi ya Wafanyabiashara jijini Nairobi (NBC) mnamo Ijumaa katika eneo la Nyamakima Bw Nyoro alisema atapanga kikao na Rais William Ruto ili kutafuta suluhu.
“Ni ukweli tuko na shida kuhusu mamlaka hizo mbili na tutahakikisha tumepata afueni. Ushuru na vita dhidi ya bidhaa ghusi ni muhimu lakini sio katika mazingira ya kuua biashara,” akasema Bw Nyoro.
Alisema kwamba amejitolea kuwa daraja kati ya wafanyabiashara hao na Rais Ruto ili kuhakikisha vita vilivyoelekezwa wachuuzi hao kati ya 2018 na 2022 havitarejelewa tena.
Mchuuzi Simon Ndirangu alisema maadui wake dhidi ya faida na kustawi ni ushuru wa juu na kuhangaishwa na askari wa kaunti almaarufu kanjo.
“Huku nikikatwa ushuru wa juu, upande huu mwingine nao kanjo wananikamata kiholela, kunipora bidhaa na kunitupa korokoroni ambapo kutoka ni baada ya kifungo au faini,” akasema Bw Ndirangu.
Maombi hayo ambayo yaliendeshwa na Askofu Harrison Ng’ang’a wa Kanisa la Christian Foundation Fellowship yalileta pamoja wanasiasa wa mirengo ya Kenya Kwanza na Azimio La Umoja-One Kenya.
Gavana Johnson Sakaja na Seneta Edwin Sifuna, mbunge wa Starehe Amos Mwago pamoja na diwani wa Jiji Bw Mwaniki Kwenya ndio walikuwa wenyeji.
Bw Mwago alidai askari wa kanjo ni kiungo cha udhalimu, akiwataka waelewe kuna haki za binadamu na pia busara ya kukinga biashara za watu kwa manufaa ya uchumi ambazo zinafaa kuwaongoza kazini.
Mrengo wa Azimio pia uliwakilishwa na kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka na aliyekuwa Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya.
Bw Kalonzo alisema kwamba anakumbuka jinsi muungano huo wa wafanyabiashara ulipenywa na kundi la fujo mwaka wa 2008 na kufanya maisha yake ya kisiasa pamoja na yale ya Raila Odinga kuwa magumu Jijini.
Bw Sakaja alisema kwamba “kuona tumeungana hivi kisiasa kuna maana kwamba kuna Mungu mbinguni ambaye ni mkuu kuliko siasa”.
Alidai utawala wa serikali iliyoondoka mamlakani ya Rais wa Nne Uhuru Kenyatta ulijiangazia kama adui wa biashara Jijini Nairobi kupitia ushuru na kudunisha mali ya wachuuzi kupitia kuiharibu kwa msingi wa vita dhidi ya bidhaa feki.
Bw Oparanya alimtaka Bw Nyoro ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya bajeti katika bunge la kitaifa aelewe kwamba “Mswada wa Kifedha (2023) ni miongoni mwa sera hasi dhidi ya wafanyabiashara na katika miaka ijayo, miswada ya aina hiyo inafaa kukwepwa”.
Bw Oparanya alisema biashara itaimarika pindi tu serikali itakuwa na upendo wa biashara za mahasla.
Bw Kalonzo aliwataka wafanyabiashara hao kukaa ngumu na waweke imani kwamba maisha yatakuwa sawa katika msingi wa bidii na kujitabiria mema.
Bw Sakaja aliahidi kwamba utawala wake unazingatia kuweka mikakati ya ushirika wa kufaana na wakazi wa Jiji la Nairobi.
Bw Kwenya alipendekeza kwamba kila Jumatatu ya kwanza ya kila mwezi iwe ikitengewa maombi ya wafanyabiashara jijini Nairobi.