Habari za Kaunti

Wafanyakazi wa kampuni iliyofurusha maskwota wajeruhiwa

January 9th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA LUCY MKANYIKA

SHUGHULI ya ubomoaji nyumba kwenye shamba la ekari 90 linalozozaniwa katika kijiji cha Msambweni, Voi, Kaunti ya Taita Taveta, imesitishwa baada ya maafisa wa usalama kuondolewa na makamanda wakuu kuhamishwa.

Aidha, wafanyakazi wawili wa kampuni ya Sparkle Properties Limited wanauguza majeraha baada ya wananchi kuwavamia walipokuwa katika harakati za kuweka ua eneo hilo lenye mzozo.

Inadaiwa wananchi wenye ghadhabu waliwavamia na kuwajeruhi wawili hao katika kijiji cha Msambweni, siku mbili baada ya ubomoaji kutekelezwa.

Afisa wa polisi ambaye hakutaka kutajwa kwa kuwa haruhusiwi kuongea na vyombo vya habari, alidokeza kuwa mfanyakazi mmoja anauguza majeraha katika Hospitali ya Rufaa ya Moi mjini Voi huku mwingine akikimbizwa Mombasa kwa matibabu zaidi.

“Tumeanzisha uchunguzi kujua waliojeruhi wafanyakazi hao. Kwa sasa bado hatujakamata yeyote kutokana na tukio hilo,” akasema.

Tukio hilo linajiri siku moja baada ya viongozi, wakiongozwa na Seneta Jones Mwaruma na Mbunge wa Voi Abdi Chome, kukabiliwa na wakazi wenye hasira wakiwalaumu kwa kushindwa kushughulikia masuala yao ya ardhi na kukosa kuingilia kati dhidi ya ubomoaji huo.

Hata hivyo, kampuni hiyo imesema kuwa itaendelea na shughuli hiyo ya kuweka mpaka katika kipande hicho cha ardhi licha ya kupingwa na wanasiasa na wenyeji.

Meneja msimamizi wa mali ya kampuni hiyo Bw Francis Mulili alisema kuwa wametafuta watu wa kulinda wafanyikazi hao wakati shughuli hiyo ikiendelea.

“Waliotekeleza unyama huo ni wahalifu na wanafaa wachukuliwe hatua kali za kisheria. Shamba ni letu na tuna haki ya kufanya mradi wowote tunaotaka,” akasema.

Bw Mulili alisema kuwa kampuni hiyo iko tayari kufanya majadiliano na wenyeji ili wanaotaka ardhi zao kubaki katika eneo hilo.

“Bado hawajakuja lakini mlango uko wazi. Kwa sasa kampuni itaendelea na mipango yake jinsi tulivyopanga,” alisema.

Ubomoaji huo ulioanza Jumamosi asubuhi wiki iliyopita ulisitishwa jioni yake baada ya Inspekta Jenerali wa Polisi Japhet Koome kuwahamisha maafisa watatu wa polisi kutoka eneo la Pwani ili kuanza uchunguzi kuhusu kisa hicho.

Maafisa hao ni Kamanda wa Polisi wa Eneo la Pwani Kenneth Kimani, Kamanda wa Polisi wa Taita Taveta Patrick Okeri, na Kamanda wa Polisi wa Voi Benastein Shari. Walitakiwa kufika Nairobi ili kuhojiwa.

Aliyekuwa kamanda wa polisi wa eneo la Kaskazini Mashariki George Sedah ameteuliwa kuwa kamanda mpya wa eneo la Pwani huku William Kiplangat akichukua nafasi ya Bw Okeri na Ibrahim Daffala akiteuliwa kuwa kamanda mpya wa polisi wa Voi.

Katika taarifa, Bw Koome aliamuru uchunguzi kuhusu mwenendo wa maafisa hao na kilichosababisha ubomoaji huo, ambao ulizua lawama kutoka kwa viongozi wa eneo hilo.

Taarifa hiyo ilisema kuwa maafisa hao watakabiliwa na hatua za kinidhamu iwapo watapatikana na makosa yoyote au matumizi mabaya ya mamlaka.

“Hatua itachukuliwa dhidi ya afisa yeyote atakayepatikana na hatia kwa kutekeleza ubomoaji huo bila idhini inayohitajika,” taarifa hiyo ilisema.

Mbunge Chome alikanusha madai kuwa anamiliki kipande cha ardhi katika eneo hilo la utata huku akisema kuwa nia yake ni kulinda wananchi dhidi ya bwenyenye huyo.

Alisema madai kuwa anamiliki kipande cha ardhi katika eneo linalozozaniwa hayakuwa na msingi.

“Kama kiongozi nimechagua amani na kuwaunganisha watu wangu, haswa wakati huu ambapo wanakadiria hasara kubwa. Similiki kipande chochote cha ardhi Msambweni. Ninamuomba yeyote aliye na ushahidi kujitokeza,” alisema.

Aidha, Gavana Andrew Mwadime alisema kuwa bwenyenye huyo hakuwa nia njema kwani alibomoa makazi hayo licha ya majadiliano kutendeka.

“Tulikuwa tunaendelea na majadiliano na tulishangaa kuwa wameanza ubomoaji. Hawakuwa na nia njema,” akasema gavana Mwadime.

Mwenyekiti wa kamati ya ardhi katika bunge la kaunti hiyo Bi Hope Anisa, aliapa kuwa serikali ya kaunti hiyo haitaidhinisha mradi wowote ambao kampuni hiyo inalenga kutekeleza katika kipande hicho cha ardhi.