Wafungwa wa kifungo cha nje kupanda miti Kilifi
NA MAUREEN ONGALA
WAHALIFU wote katika Kaunti ya Kilifi watakaopewa adhabu ya kifungo cha nje kupitia idara ya urekebishaji tabia watalazimika kupanda miti ili kuongeza idadi ya misitu.
Haya ni kulingana na kamishna wa Kaunti ya Kilifi Bw Josephat Biwott.
Kulingana na Bw Biwott ni kuwa idara ya usalama Kaunti ya Kilifi imekubaliana na mahakama, Ofisi ya Kiongozi wa Mashtaka ya Umma (ODPP), maafisa wa Shirika la Misitu nchini (KFS) na wale wa kurekebisha tabia na wadau wengine ya kwamba kila mfungwa wa kifungo cha nje atapanda miti isiyopungua 100.
Akizungumza baada ya shughuli ya kupanda miti katika gereza la Bofa mjini Kilifi, Bw Biwott alisema kiwango cha miti katika kaunti ya Kilifi kimepungua marudufu kutoka asilimia 35 hadi 27.
“Tumepoteza takriban asilimia nane (8) ya misitu na tumeamua ya kwamba iwapo tutakukamata ikiwa unaharibu misitu hatutakuonea huruma. Tutakushtaki na mwishowe lazima upande miti,” akasema Bw Biwott.
Alisema uharibifu wa misitu uko katika kiwango ya juu Kilifi kutokana na uchomaji wa makaa.
Kamshna Biwott alisema misitu iliyoharibiwa kwa kiwango kikubwa ni ile ya kibinafsi na mashamba ambayo serikali hupeana kwa maskwota.
“Unapata wananchi wanapewa mashamba yakiwa na misitu lakini wanaanza kukata miti kuchoma makaa ardhi ikibaki kavu,” akasema.
Aidha alisema kuwa kuendelea mbele, serikali itatenga asilimia 10 ya ardhi kwa kila mashamba yatakayopeanwa kwa maskwota. Wakianza na ekari 9,000 za shamba lililoko Bomani.
Bw Biwott alisema kuwa misitu hiyo itaorodheshwa rasmi katika Gazeti Rasmi la Serikali kupitia serikali ya kaunti ya Kilifi ili kulindwa na kutunzwa.
Kiongozi huyo wa utawala aliwaonya wanaoendeleza biashara ya makaa kuwa chuma chao ki motoni.
Alisisitiza wahudumu wa bodaboda wanaosafirisha magunia ya makaa kila siku kuelekea mijini watanyakwa.
Alisema wanaokata miti na kuchoma makaa hutumia bodaboda kusafirisha bidaa hiyo hadi katika masoko yao.
Aidha Bw Biwott aliwalaumu maafisa husika kwa kutowajibika katika kuwachukulia hatua za kisheria bodaboda wanaosafirisha makaa.
“Wale wanaharibu misitu wanatumia pikipiki.Ukiwa barabara unakutana na bodaboda wamebeba makaa gunia kumi huku tukiangalia bila kuchukua hatua na ni hasara tuendelee kupanda huku wengine wakiaribu,” akasema.
Pia wale wahalifu watakaoshtakiwa kwa kuchoma makaa na kusafirisha watapanda miti kama adhabu.
Onyo hilo la kamishna wa kaunti ya Kilifi linatotolewa huku biashara ya makaa ikiendelea kunoga katika kaunti ya Kilifi na hata jiji kuu la Nairobi.
Hata hivyo, bodaboda wanaosafirisha magunia ya makaa kuelekea mijini wamedai kuhangaishwa na maafisa wa polisi, maafisa wa Idara ya Huduma kwa Wanyamapori (KWS) na wale wa KFS wanaotaka kitu kidogo kutoka kwao.
Licha ya kuwa bodaboda wanaosafirisha makaa kuhatarisha maisha yao na ya wenzao kwa kuwabeba juu ya magunia ya makaa, wao hupita katika vizuizi vya polisi barabarani.
Maeneo ya Kaloleni, Ganze na Magarini yamejulikana kwa kuchoma makaa.
Mwanaharakati wa uhifadhi wa misitu katika kaunti ya Kilifi Bw Elvis Fondo alisema kuwa idadi kubwa ya misitu imeharibiwa kutokana na ongezeko na mabadiliko ya matumizi ya miti kutoka kwenye misitu hadi mashamba.
Hata hivyo, alisema idara hiyo ya misitu inaendeleza hamasisho kwa jamii kuhusu kuhifadhi misitu.