Wahubiri Mombasa nao pia wapinga Mswada wa kudhibiti makanisa
VIONGOZI wa kidini katika Kaunti ya Mombasa, wamejiunga na wenzao nchini kupinga Mswada uliopendekezwa wa Mashirika ya Kidini wa 2024.
Kulingana nao, mswada huo unakiuka uhuru wa kuabudu kwani baadhi ya mapendekezo yanalenga kudhoofisha nafasi ya kanisa katika jamii.
Wameitaka kusimamisha mchakato mzima utakaopelekea utekelezaji wa mpango huo hadi ushirikishwaji wa umma ufanyike kikamilifu kote nchini na maoni yao yakusanywe.
“Kama kanisa tunapinga kikamilifu Mswada wa Mashirika ya Kidini wa 2024 kwa sababu tunahisi hili ni sawa na kudharau taasisi za ibada na ni ukiukaji wa moja kwa moja wa haki zetu za kikatiba kuhusu uhuru wa kuabudu,” alisema Mchungaji Peter Onyango wa Kanisa la United Chapel lililo Changamwe, Kaunti ya Mombasa.
Wahubiri hao chini ya muungano wa Mombasa Pastors Fellowship waliongeza kuwa, waliounda mswada huo hawakufuata taratibu zinazofaa za kisheria.
“Tunaomba serikali ichukue tahadhari kubwa. Isikilize maoni ya makasisi na iondoe mswada huu. Sisi ni taifa linaloomba na tukiamua kuomba watatambua nguvu ya maombi,” akasema Askofu Tee Nalo wa Kanisa la Praise Chapel lililo eneo la Kizingo.
Mswada huo unapendekeza kuanzishwa kwa afisi ya msajili wa mashirika ya kidini, ambaye atasimamia utoaji na kufuta vyeti, kutunza sajili ya mashirika yote ya kidini, pamoja na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika taasisi zote za kidini nchini ili kuhakikisha zinafuata masharti.
“Tunaiambia serikali ikae mbali na masuala ya kanisa. Mkiingilia kanisa basi tutaamua kuomba na tukifanya hivyo sote mtajua kweli nguvu ya maombi,” alisema Mchungaji Gabriel Gimel wa Kanisa la Imani Baptist lililo Maweni.
Kulingana na mswada huo, hakuna mtu atakayeruhusiwa kubadilisha au kuhamasisha mwingine kutoka dini moja kwenda nyingine kwa ushawishi usiofaa au kwa kulazimisha, kutumia dini kukiuka haki za watoto, au kutoa mafundisho ya kidini kwa mtoto bila idhini ya mzazi au mlezi wake.
Ukiukaji wa masharti haya ni kosa linaloadhibiwa, endapo mtuhumiwa atapatikana na hatia, kwa faini isiyozidi Sh10 milioni, kifungo kisichozidi miaka mitano, au vyote viwili.
Mnamo Julai, Baraza la Mawaziri liliidhinisha mapendekezo kutoka kwa Jopokazi la Rais kuhusu Mashirika ya Kidini ili kulinda uadilifu wa utekelezaji wa dini.
Mageuzi yaliyopendekezwa yaliandaliwa kufuatia janga la Shakahola ambapo zaidi ya watu 400 walikufa kwa njaa wakiamini walikuwa wakifunga ili wakutane na Yesu.
Baraza la Mawaziri lilieleza kuwa, mswada uliopendekezwa unaunganisha udhibiti wa ndani wa mashirika ya kidini kupitia mashirika yao ya kidini, pamoja na usimamizi kutoka kwa taasisi za serikali kama vile vyombo vya usalama.