Habari za Kaunti

Wakazi wa Kangai wateketeza baa ya mauti

February 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA GEORGE MUNENE

WAKAZI wenye ghadhabu wameteketeza baa ambako watu sita Jumanne waliaga dunia huku watano wakipofuka macho kwa muda baada ya kubugia pombe inayodaiwa kuwa na sumu katika kijiji cha Kangai, Kaunti ya Kirinyaga.

Wakazi mnamo Jumatano alfajiri wameteketeza baa hiyo ya bwanyenye wa eneo hilo huku idadi ya waliopoteza maisha yao ikigonga 10 baada ya wanne zaidi kuzidiwa na maumivu.

Mali ya maelfu imeharibiwa.

Taifa Leo imepata kreti za bia, chupa na meza zikiwa zimetapakaa.

Polisi walipata kama mali nyingi ndani ya baa hiyo ikiwa imeteketea na kuwa majivu.

Inadaiwa kwamba walevi waliingia kwa baa hiyo mnamo Jumatatu usiku ambapo walibugia pombe hiyo huku wakipiga gumzo.

Walikunywa hadi wakalewa kisha wakaondoka mmoja baada ya mwingine kurudi majumbani mwao.

Lakini Jumanne asubuhi walevi hao walianza kulalamikia maumivu ya tumbo.

Kufika mchana, watu watano walikuwa wameaga dunia. Mwingine mmoja aliaga dunia mara baada ya kufikishwa katika hospitali ya Kerugoya ambako alikimbizwa na jamaa.

Waziri wa Michezo, Utamaduni na Huduma za Kijamii wa Kaunti ya Kirinyaga Dennis Muciimi alisema bodi ya kupeana leseni ilipuuza ombi la baa hiyo mnamo Desemba 2023.

“Baa hiyo ilishindwa kuzingatia sheria ya kudhibiti pombe nambari 3 ya mwaka 2014,” akasema Bw Muciimi.

Naye mwenzake wa Afya George Karoki alisema watano waliokuwa wamepofuka walikuwa wakipokea matibabu katika kituo cha huduma za afya cha Njegas.

Soma Pia: Watu sita waaga dunia, watano wapofuka baada ya kubugia pombe ya sumu

Dkt Karoki alisema wagonjwa hao walifikishwa hospitalini wakiwa na dalili za kuona vimulivuli ishara ya kumaanisha walikuwa na natatizo ya mapafu na mfumo wa neva.

“Tunashuku walikunywa pombe yenye kiwango kikubwa cha kemikali ya ethanol inayoleta madhara kwa mapafu,” akasema Dkt Karoki.

Naye Naibu Kamishna wa Mwea Magharibi Teresia Wanjiku alisema mmiliki wa baa hiyo amekuwa akikamatwa mara kwa mara na kushtakiwa kwa kuuza pombe haramu lakini akiachiliwa kwa sababu ya ukosefu wa ushahidi wa kutosha.

Afisa huyo alitaja kisa hicho kuwa cha kufedhehesha.

Alijitetea kwamba maafisa wake wamekuwa wakijaribu kuzuia mkasa huo kupitia kuvamia baa hiyo ya California.

“Lakini juhudi zetu zimekuwa zikiambulia patupu kupitia ilani za mahakama za kutuzima kumtia mbaroni mmiliki na kufunga baa yake,” akasema Bi Wanjiku.