• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 2:00 PM
Wakazi wa Whitehouse kubomolewa nyumba zao kupisha mradi wa nyumba za bei nafuu

Wakazi wa Whitehouse kubomolewa nyumba zao kupisha mradi wa nyumba za bei nafuu

NA SIAGO CECE

ZAIDI ya wakazi 2,000 wa mtaa wa Whitehouse ulioko eneo la Diani katika Kaunti ya Kwale wamepinga vikali mpango wa serikali wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu katika eneo hilo.

Haya yanajiri kufuatia hatua ya serikali ya kaunti hiyo ya kutaka kutekeleza mradi huo wa serikali kuu katika ardhi ya eneo hilo la ekari sita.

Familia hizo zaidi ya 500 sasa zinaishi katika hofu ya kubomolewa nyumba zao ambazo wanasema wameishi hapo kwa zaidi ya miaka 30.

Mtaa wa Whitehouse umejengwa katika ardhi ya ekari sita, na ni dakika chache tu karibu na ufuo wa Diani. Ifahamike kwamba Diani ni mji wa kitalii.

Wengi wa wakazi  wanaoishi katika nyumba hizo zaidi ya 500 wanafanya kazi katika sehemu za kutalii za mji huo, huku biashara zikinoga kutokana na wingi wa watu wanaoishi hapo.

Baadhi ya wanachama wa kikundi cha wakazi wa mtaa wa Whitehouse wakiwa katika kikao cha majidiliano. Walidai walipokea habari kuhusu mradi wa mtaa huo kupitia vyombo vya habari. PICHA | SIAGO CECE

Kulingana na mwenyekiti wa kikundi cha wakazi hao wa Whitehouse Bw Francis Muthoka, hatua ya serikali kujenga nyumba hizo kwa ardhi hiyo itakuwa kuwadhulumu wakazi wa hapo ambao wengi hawana makao mengine.

“Tulipewa ardhi hii na serikali ya kaunti miaka 40 iliyopita na tumekuwa tukilipa kodi tangu wakati huo. Wakazi hapa walitakiwa kujenga nyumba zao wenyewe na tulizijenga na pia kuwekeza katika biashara. Sasa tunaarifiwa kuwa zote zitabomolewa,” Bw Muthoka akasema.

Baada ya kupokea sehemu hiyo, Bw Muthoka alikuwa kati ya wafanyabiashara wa kwanza kufungua maduka yao hapo, yeye akiita lake Whitehouse, ambalo liliishia kuwa jina la mtaa huo.

Kwa upande wake, Bi Monika Mutio alisema kuwa ikiwa mpango wa serikali utaendelea, atakosa makao, kwani hakutakuwa na fidia yoyote ambayo wakazi watapewa.

Bi Monika Mutio, mmoja wa wakazi wa Whitehouse katika mahojiano na Taifa Jumapili. Alieleza kuwa amekuwa mmiliki wa nyumba kwa muda mrefu. Aliomba serikali kuwasikiliza wakazi. PICHA | SIAGO CECE

“Nimeishi hapa tangu nikiwa msichana mdogo nikifanya biashara. Nyumba ambayo nilijenga katika ardhi hii, nimekuwa nikilipa kodi kwa serikali. Sasa sina pa kuenda ikiwa mradi huu utaendelea,” akasema Bi Mutio.

Naye Tirus Muriku alisema wakazi wengi wanalipa madeni kwenye benki baada ya kuchukua mikopo ili kufanya ujenzi hapo, wakiwa na matumaini ya kupata hatimiliki.

Kulingana na wakazi, wamekuwa wakilipa kodi ya Sh6,000 kila mwaka kwa ardhi hiyo ya serikali ya kaunti, huku barua walizopewa za ardhi hiyo zikieleza kuwa watapata hatimiliki ya ardhi.

Lakini Kamishna wa Kaunti ya Kwale Micheal Meru, ambaye ni mwenyekiti wa kamati inayohusika na mpangilio wa nyumba hizo, alithibitisha kuwa mradi wa nyumba za bei nafuu Kwale utaendelea, na unatarajia kuanza wiki mbili zijazo.

Maeneo mengine, yakiwemo ya Kwale Housing Scheme, Kwale Survey Camp, na Mabokoni Smart City pia yamechaguliwa kwa ujenzi wa zaidi ya nyumba 10,000 za serikali.

Hatua hiyo pia iliungwa mkono na gavana wa Kwale Fatuma Achani ambaye alisema kuwa lengo kuu ni kuhakikisha kila mkazi wa Kwale ameweza kuishi kwe nidhamu kwa bei nafuu.

Kulingana na Waziri wa Ardhi Kwale Saumu Beja, ombi la gavana kwa serikali ni kuwa wakazi na wafanyibiashara watapewa kandarasi za ujenzi huo ili kufaidi na mradi.

Alieleza kuwa serikali ya kaunti imepatia serikali kuu ardhi hiyo ili mradi hufanyika hapo.

Wakazi hao sasa wameitaka serikali ya Kwale kutafuta sehemu mbadala ya ujenzi wa nyumba hizo au iwafidie kwa uwekezaji ambao wameweka katika ardhi hiyo.

“Kuna vipande vingi vya ardhi hasa karibu na fuo za bahari ambavyo havijamilikiwa kwa zaidi ya miaka 50. Kwa nini tunadhalilishwa na kutaka kutolewa sehemu hii?” mkazi mwingine akauliza.

  • Tags

You can share this post!

Wenye baa wataja sababu za kuajiri mabaunsa nyamaume

Saratani: Himizo wanaume wapimwe

T L