• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Wakazi wa Witeithie watibiwa macho bila kutoa senti

Wakazi wa Witeithie watibiwa macho bila kutoa senti

NA LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa Witeithie, Juja walifurahia matibabu ya bure ya macho yaliyotolewa kupitia mpango uliofadhiliwa na Chuo Kikuu cha Zetech, serikali ya Kaunti ya Kiambu, kanisa la PCEA Kikuyu, na hospitali ya Christian Blind Mission for Transformative Eye Medical Clinic.

Wakazi zaidi ya 1,000 kutoka kijiji hicho walifurika katika bewa la Mang’u la Zetech kwa matibabu hayo ya bure.

Wakongwe ni miongoni mwa wagonjwa wa macho waliofika kupokea matibabu.

Zetech mbali na masomo, imepiga hatua na kujihusisha kikamilifu na masuala yanayohusu afya ya wananchi.

Kulingana ni utafiti uliofanywa na Christian Blind Mission, Wakenya wapatao 7.5 milioni wanastahili kukaguliwa macho kutokana na maradhi ya macho lakini wanaokaguliwa ni 1.6 milioni pekee.

Imefichuka wengi wao hukosa fedha za kulipia matibabu hayo na wengine hukosa kufanyiwa ukaguzi kwa sababu hawana habari kuwa wanastahili kuona daktari.

Baadhi ya wakazi wa Witeithie, Juja, waliofika katika Chuo Kikuu cha Zetech kupata matibabu ya macho. PICHA | LAWRENCE ONGARO

Naibu Chansela wa Zetech Prof Alice Njuguna alipongeza ushirikiano walioweka na washika dau wengine akisema utaboresha zaidi matakwa ya wananchi popote walipo.

“Tutahakikisha chuo chetu kinaendeleza mipango yake ya kujali wananchi wa mashinani kwa kuwapa matibabu ya bure kila mara katika maeneo tofauti,” alisema Bi Njuguna.

Alisema kwa ushirikiano na washikadau wengine, chuo hicho kitaendelea kuonyesha ukarimu wake kuhakikisha kinajali maslahi ya mwananchi.

“Tunaomba serikali na madaktari kumaliza mkwamo ili mgomo uishe na warejee kazini kushughulikia wagonjwa,” alisema msomi hiyo.

Alisema ajenda ya Zetech ya 2014- 2030 inatilia maanani kujali maslahi ya wananchi kwa maswala mengine tofauti.

Afisa wa afya wa kaunti Ndogo ya Juja Bi Anne Mwangi, alisema matatizo ya maradhi ya macho yanatokana na maswala ya mazingira kama kuingiwa na vumbi na utumizi wa vifaa vya mtandao kama kompyuta na simu kwa muda mrefu.

Alisema Kaunti ya Kiambu itaendelea kuungana na Zetech ili kujali wananchi kwa kutoa huduma muhimu za afya.

  • Tags

You can share this post!

Msupa akerwa na jombi wake kujitoa mapema baada ya polo...

Ulegevu wa polisi unavyochochea ghasia za kisiasa Kisii

T L