Habari za Kaunti

Wakili aitwa kueleza madai kwamba serikali inapanga ‘kuua Mackenzie jela’

Na BRIAN OCHARO September 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MKUU wa gereza la Shimo La Tewa ameagizwa kufika mahakamani kujibu madai kwamba serikali inapanga kumuua mshukiwa wa mauaji ya Shakahola, Paul Mackenzie, kwa kumtilia sumu kwenye chakula.

Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Watoto ya Tononoka, Bi Nelly Chepchirchir, alitoa maagizo hayo Jumanne baada ya Mackenzie kudai maisha yake yamo hatarini.

Aidha, aliagiza kuwa katika kipindi kilichosalia cha kesi mahakamani, wakati washtakiwa wanapopewa chakula, mgao wa chakula cha Mackenzie usimamiwe na wahudumu wa mahakama.

“Mackenzie atapewa chakula chake cha maziwa na mkate ambacho atakula mbele ya wakili wake na afisa wa mahakama,” aliagiza hakimu.

Mackenzie alidai kuwa, alipata unga mweupe katika sehemu ya kuwekea mdomo kwa chupa yake ya maji ya kunywa na vilevile katika eneo anakokula mara kwa mara.

Alidai pia kuwa, alipata vipande vya chupa vilivyosagwa kando ya eneo lake la kula vikiwa vimepakiwa vizuri, akiamini ni kwa nia ya kumuua.

Wakati uo huo, hakimu alimwelekeza Mackenzie kuwasilisha ombi rasmi katika mahakama husika yenye mamlaka ya kusikiliza masuala yanayohusu haki.

Mahakama pia ilimwelekeza Mackenzie, kupitia wakili wake Lawrence Obonyo, kuwasilisha malalamishi rasmi kwa polisi.

Bi Chepchirchir pia aliamuru vielelezo vilivyowasilishwa ikiwemo chupa ya maji ambayo haijafunguliwa na karatasi mbili zilizokunjwa zikiwa na vipande vya kioo kilichovunjika, vihifadhiwe na Bw Obonyo hadi uchunguzi ukamilike baada ya kutoa taarifa kwa mujibu wa agizo la mahakama.