Habari za Kaunti

Wakulima wa korosho kufaidi kwa kiwanda kipya

March 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WAKULIMA wa korosho katika Kaunti ya Lamu wanatarajia kufaidika na mpango wa kujenga kiwanda cha korosho eneo hilo.

Hii ni baada ya Gavana Issa Timammy na Balozi wa Uingereza nchini Kenya, Neil Wigan, kuweka jiwe la msingi kwa ujenzi wa kiwanda hicho.

Kwa mujibu wa Ubalozi wa Uingereza, mpango huo unalenga kuunda nafasi za kazi na kuwawezesha wakulima kupata faida zaidi kutokana na mazao yao.

“Tumeanza mpango wa ujenzi wa kiwanda cha kwanza cha korosho katika Kaunti ya Lamu ambacho kitafadhiliwa na serikali ya Uingereza na kutoa nafasi za ajira kwa wenyeji,” akasema Bw Wigan, kwenye hafla hiyo ya Jumatano.

Kwa upande wake, Bw Timammy alisifu hatua hiyo akisema itasaidia katika azimio la kuhakikisha kuwa wakulima wanapata faida kutoka kwa mazao yao kupitia uchakataji na uongezaji wa thamani.