• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 5:04 PM
Wakulima wa miraa wahangaika kufuatia watumiaji kuhamia kwa ‘Muguka’

Wakulima wa miraa wahangaika kufuatia watumiaji kuhamia kwa ‘Muguka’

NA DAVID MUCHUI

WAKULIMA wa miraa katika Kaunti ya Meru sasa wanaitaka serikali kuharakisha mikakati ya ufufuzi wa kilimo cha zao hilo, kwani bei zake zinaendelea kushuka.

Kwa miezi mitatu iliyopita, bei za zao hilo zimeshuka kutoka Sh50,000 kwa gunia la kilo 100 hadi Sh15,000 katika siku za hivi karibuni, hali ambayo imezua kilio miongoni mwa wakulima.

Wafanyabiashara sasa wanahusisha hali hiyo na uwepo wa makateli, wanaonunua kilo moja ya zao hilo kwa Sh828.

Wanasema hali hiyo imeathiri sana uuzaji wa zao hilo na kuzua ushindani kutoka kwa ‘Muguka’, ambao ni aina nyingine ya miraa inayokuzwa katika Kaunti ya Embu.

Hali ya kushuka kwa bei hizo pia ilithibitishwa na Waziri wa Klimo, Mithika Linturi, mnamo Jumapili, ikizingatiwa kuwa hata yeye ni mkulima wa miraa.

Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha televisheni, Bw Linturi alisema kuwa mnunuzi mmoja alikuwa akimpendekezea bei ya Sh50,000 kwa miraa aliyomuuzia Sh380,000 hapo awali.

Kulingana na Chama cha Wakuzaji Miraa cha Nyambene (Nyamita), watumiaji wengi wa miraa wameamua kutumia njia mbadala kutokana na kupungua kwa hitaji la zao hilo, licha ya uwepo wake kwa wingi.

Wafanyabiashara wanaouza zao hilo katika nchi za nje wameamua kupunguza bei wanazoinunua kutoka kwa wakulima, ili kufidia ‘ada za makateli’ wanazoitishwa kabla ya ndege ya kuisafirisha nje ya nchi kuondoka.

Kutokana na hali hiyo, mamia ya wakulima wa miraa katika Kaunti ya Meru wamekuwa wakifanya maandamano tangu wiki iliyopita, kulalamikia kushuka kwa bei za zao hilo.

Licha ya wakulima kuyalaumu makateli kutokana na kushuka kwa bei za zao hilo, mwenyekiti wa Nyamita, Bw Kimathi Munjuri, anasema kuna hitaji wakulima kupanga upya soko lake nchini, serikali inapoendelea kuimarisha soko lake katika mataifa ya nje.

“Baada ya janga la Covid-19, Somalia iliweka masharti makali ambayo yalipunguza kiwango cha miraa tunayouza katika taifa hilo hadi tani 20 kwa siku. Hilo liliwaacha wengi wetu bila soko la zao hili,” akasema Bw Munjuri.

Kwa muda mrefu, Somalia ndiyo imekuwa soko kuu la zao hilo kutoka Kenya.

Bw Munjuri pia alitaja kushuka kwa bei la zao hilo kuchangiwa na mabadiliko ya mahitaji ya watumiaji wake na ushindani mkali kutoka kwa Muguka.

  • Tags

You can share this post!

Maswali yaibuka Gavana Mwadime ‘Wakujaa’...

Alan Shearer: Mtarajie mabadiliko juu ya jedwali la EPL...

T L