Habari za Kaunti

Wakulima wa ndizi wanavyohangaika kupata soko mazao yakiozea shambani

March 11th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA KALUME KAZUNGU

WAKULIMA wa ndizi katika kisiwa cha Pate, Lamu Mashariki wanaililia serikali ya Kaunti, ile ya kitaifa na wadau mbalimbali kuwatafutia soko la zao hilo linalofanya vyema kwa sasa.

Kisiwa cha Pate kwa miaka mingi sasa kimekuwa kikivuna ndizi kwa wingi huku wakulima wakikosa soko la kutegemewa kwa zao hilo.

Wakizungumza na Taifa Leo Dijitali kisiwani Pate mwishoni mwa juma, wakulima walisema tegemeo lao la pekee kuuza ndizi ni soko la Manispaa ya Lamu lililoko katika kisiwa cha Lamu ambako ni mbali.

Ahmed Haji, mmoja wa wakulima wa ndizi, alisema kila msimu wanapovuna matunda hayo huishia kuyauza rejareja mjini humo zingine zikisafirishwa kwa boti kupelekea wachuuzi wa soko la Manispaa ya Lamu.

Kulingana na Bw Haji, kusafirisha shehena ya ndizi kutoka Pate hadi kisiwa cha Lamu kwa boti ni ghali.

Wakulima hao hutakiwa kulipa nauli ya kati ya Sh20,000 na Sh40,000 kusafirisha shehena ya ndizi na mizigo mingine kutoka Pate hadi mjini Lamu kutumia mashua au boti kubwa.

Bw Haji aliomba wahisani kujitokeza na kuwaanzishia kiwanda cha kutengeneza na kuzidisha ubora wa ndizi ili kusaidia wakulima wa eneo hilo kujipatia soko mahali walipo.

“Kama uonavyo sisi wakazi wa Pate wengi wetu ni wakulima. Karibu kila pembe ya kisiwa hiki utapata migomba iliyonawiri vilivyo. Karibu kila mgomba hapa una mkungu mkubwa wa ndizi. Endapo hizi ndizi uonazo zitaiva kwa wakati mmoja basi zitaishia kutuozea hapa kama ilivyo ada.

“Ni ombi letu kwamba kaunti na serikali kuu watatutafutia soko maalumu kutuwezesha sisi wakulima kupata mtaji kutokana na kilimo hiki. Pia wanaweza kutuanzishia kiwanda cha ndizi hapa,” akasema Bw Haji wakati wa mahojiano.

Bi Fatma Bakari, mkulima mwingine, alisema kukosekana kwa soko la kutegemewa kuuza ndizi ndicho kizingiti kikuu kinachozuia kupanuliwa kwa kilimo cha ndizi kisiwani Pate.

Licha ya wakulima kuwa na ari ya kukuza migomba, wengi wao huishia kuvunjika moyo kutokana na kukosekana kwa soko maalumu la zao hilo.

“Tungekuwa na kiwanda cha ndizi hapa Pate au soko la kutegemewa kwa ndizi, basi hiki kilimo cha migomba hakingekuwa jinsi kilivyo. Hii sekta ingepanuka pakubwa. Kukosekana kwa miundomsingi kama soko au kiwanda ndiyo sababu ya sekta ndogo ya kilimo cha ndizi kutopanuka Pate na Lamu Mashariki kwa jumla,” akasema Bi Bakari.

Kauli yake iliungwa mkono na Bw Mohamed Hassan aliyesisitiza kuwa kama vile wakulima wa korosho wanavyoanzishiwa kiwanda cha korosho mahali kama Hindi, Lamu Magharibi, vile vile wakulima wa ndizi kisiwani Pate, Lamu Mashariki pia wakumbukwe kwa miundomsingi sawia.