Habari za Kaunti

Wakulima wa viazi pazuri kaunti ikijenga kiwanda

Na ERIC MATARA August 30th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WAKULIMA wa viazi katika Kaunti ya Nakuru na zile za karibu wanatarajia kufaidi pakubwa baada ya mwekezaji mmoja kutangaza kuwa ataanzisha kiwanda cha viazi katika eneo maalum ili kuendeleza shughuli za kiuchumi, Naivasha (NSEZ).

Kampuni hiyo, Crystal Frozen and Chilled Foods Ltd, ni ya tatu kukita kambi katika eneo la kiviwanda la Maai Mahiu.

Kiwanda hicho cha kusindika viazi kitaanza kufanya kazi ndani ya kipindi cha miezi sita ijayo.

Kiwanda hicho, kitakuwa kikisindika kilo milioni moja ya viazi kila mwezi na kinatarajiwa kutoa soko kwa wakulima wa zao hilo katika kaunti za Nakuru na Nyandarua zinazozalisha viazi kwa wingi.

Crystal Frozen and Chilled Food Ltd, itasaidia kumaliza visa vya kuharibika kwa viazi ambavyo kwa miaka mingi vimeathiri wakulima, haswa katika kaunti za Kusini mwa Bonde la Ufa.

“Kampuni hiyo ya viazi italeta mwamko mpya katika kilimo cha viazi. Kitazalisha nafasi 359 za moja kwa moja za ajira kwa vijana na wanawake kulingana na ajenda ya kiuchumi ya serikali ya Kenya Kwanza,” Gavana Susan Kihika akasema.

Kulingana na mkurugenzi wa kampuni hiyo, Bw Mungai Kihuyu, kitasindika zaidi ya kilo milioni tano ya viazi kwa mwezi katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Aidha, kampuni hiyo, Bw Kihuyu alisema, inashirikiana kwa karibu na Chuo Kikuu cha Egerton katika kuendesha utafiti ili kusasaidia wakulima kupata mbegu bora kwa mapato bora.

Wakulima wa viazi wamekuwa wakilalamikia kuhangaishwa na mabroka na mawakala, licha ya kaunti zinazokuza zao hilo kubuni sheria ya upakiaji.