• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 1:01 PM
Wakulima wapinga bei ya mbolea ya gharama nafuu

Wakulima wapinga bei ya mbolea ya gharama nafuu

NA SHABAN MAKOKHA

WAKULIMA katika kaunti ya Kakamega wamekataa mbolea ya bei nafuu iliyotolewa na kaunti hiyo wakidai bidhaa hiyo inauzwa kwa bei ghali.

Wamesema hayo wakati ambapo baadhi ya wanasiasa katika kaunti hiyo kuitaka Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kuchunguza jinsi Gavana Ferdinand Barasa anavyotumia pesa za umma.

Malalamishi hayo yanajiri baada ya Gavana Barasa kuzindua usambazaji wa mbolea hiyo ya thamani ya Sh712 milioni.

Mbolea hiyo inauzwa kwa magunia ya uzani wa kilo 25 na kilo 50.

Mbolea ya kilo 25 inauzwa kwa Sh1,920 ilhali ile ya kilo 50 inauzwa kwa Sh3,800, ambayo ni Sh1,300 zaidi ya bei mbolea iliyotolewa na serikali ya kitaifa.

Mbejeo nyingine zinazosambazwa na serikali ya kaunti ya Kakamega ni kama vile mbegu, lishe ya Samaki na madini mengine ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya shambani.

Gavana Barasa alisema kuwa kaunti hiyo imenunua magunia 120,000 (ya kilo 25) ya mbolea ya upanzi, magunia 120,000 (ya kilo 25) ya mbolea ya kuweka baada ya mimea kuchipuka na paketi 103,240 za kilo mbili za mbegu ya mahindi iliyoidhinishwa.

“Stoo zote katika kaunti ya Kakamega zitakuwa zimepokea pembejeo mbalimbali kufikia mwishoni mwa wiki ijayo ili wakulima wazinunue kwa msimu wa upanzi,” akasema Bw Barasa alipozindua shughuli ya usambazaji wa mbolea katika sehemu kadhaa za maeneo bunge ya Butere na Shinyalu.

Katika Kaunti ndogo ya Shinyalu, Bw Barasa na maafisa wake walisambaza magunia 9,000 ya mbolea ya upanzi, magunia 9,000 ya mbolea ya kutumika baada ya upanzi na paketi 8,000 za mbegu za mahindi zilizoidhinishwa.

Katika eneobunge la Butere, wakulima walipokea magunia 7,500 ya mbolea ya upanzi, magunia 7,500 ya mbolea ya kuweka baada ya upanzi na paketi 7,500 za mbegu za mahindi zilizoidhinishwa.

“Bei ya gunia moja ya kilo 25 ni Sh1,920 ya mbolea ya upanzi, Sh1,350 kwa kila moja ya gunia la mbolea ya ‘top dressing’ na Sh305 kwa kila moja ya paketi ya kilo mbili ya mbegu ya mahindi iliyoidhinishwa,” akasema Bw Barasa.

Mkuu huyo wa kaunti aliongeza kuwa mbolea ya gharamu nafuu ndio suluhu kwa shida ya kudorora kwa madini faafu kwenye udongo katika kaunti ya Kakamega.

Hii ni kwa sababu mbolea hiyo imenunuliwa baada ya udongo kufanyiwa ukaguzi wa kina.

Ili kununua bidhaa hizo, ikiwemo lishe ya samaki ya thamani ya Sh9 milioni, wakulima wanashauriwa kufika katika afisi za wadi ambako maafisa wa kilimo katika ngazi hiyo watatoa ushauri wa kitaaluma.

  • Tags

You can share this post!

Kenya yachagua kikosi cha kuteka dunia mbio za nyika

Viongozi waambiwa waachie asasi maalum vita dhidi ya pombe

T L