Walalamishi wakwepa machifu wanaoelewa mizozo yao
NA KALUME KAZUNGU
KUMEIBUKA mtindo mpya wa wakazi wa maeneo mengi Lamu kukwepa machifu na badala yake kuanzia afisi za juu kutafuta huduma.
Badala ya kuwaendea machifu, raia hao hufululiza kwa Naibu Kamishna au Kamishna.
Machifu wanalalamika kuwa hayo hutokea sana punde walalamishi –wale ambao si wakweli–wanapogundua kuwa chifu yuko na ukweli na ufahamu au historia fulani kulihusu jambo linalopiganiwa au kuzozaniwa.
Wanasema kwamba raia hao mara nyingi huishia kugonga mwamba huko juu, ambapo huagizwa warudi chini (kwa machifu) kutatua mzozo husika.
Kesi hasa zile zinazofungamana na utata wa ardhi mara nyingi ndizo ambazo watu wanakwepa kwenda kwa machifu wao wakijua ni wajuzi wa historia na ufahamu kuhusu ardhi hizo.
Aidha, afisi za machifu eneo hilo hazijashikika kwa shughuli za kila siku katika kuwahudumia wananchi.
Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo aidha ulibaini kuwa wananchi wengi wanaoendeleza tabia hizo ni wale ambao wanafahamu fika kuwa machifu wao wako na ukwasi wa ufahamu au historia kuhusiana na jambo fulani wanalotafuta usaidizi au utatuzi kulihusu.
Baadhi ya maafisa wa utawala waliozungumza na Taifa Leo walisema raia wengi, hasa wale wenye mizozo inayohusiana na mashamba, mara nyingi hawapendelei kutafuta utatuzi wa migogoro hiyo kwa machifu wao mitaani.
Badala yake, wananchi hao wamekuwa wakizuru afisi za manaibu kamishna au hata ile ya kamishna wakidhania kuwa huko ndiko watapata utatuzi wa hakika.
Chifu Mkuu wa Mpeketoni Philip Githinji hata hivyo alishukuru mpangilio uliopo wa kiutawala, ambapo wananchi wanaotorokea kutafuta utatuzi wa mizozo yao kwenye afisi za utawala za ngazi za juu wameishia kurudishwa kujadili na kutatua mizozo yao katika afisi za machifu.
“Pindi mwananchi anapogundua kuwa chifu wake yuko na ufahamu wa kweli au historia ya kutosha kulihusu jambo fulani analopigania au kuzozania, tayari anaanza kumwangalia chifu wake kivingine,” akasema Bw Githinji.
Aliongeza, “Wengine hata wanajua wao ndio wenye makosa na wanaogopa haki itendeke. Hapo ndipo utapata wamekwepa afisi za machifu na kukimbilia zile za ngazi za juu kama vile kwa naibu kamishna au kamishna. Ila cha kufurahisha ni kwamba raia hao huishia kugonga mwamba huko juu kwani huagizwa warudi huku chini kwa machifu waliowadharau ili kutatua mizozo yao.”
Maafisa hao wa utawala pia wamelalamikia tabia za baadhi ya raia ambao huwaona machifu kuwa watu dhaifu, hivyo kudharau kabisa huduma zao muhimu wanazotekeleza katika jamii.
Baadhi ya majukumu ya machifu nchini ni kuhakikisha kuna utiifu wa sheria miongoni mwa wananchi au raia kwenye maeneo yao ya utawala.
Pia wana uwezo wa kuchagua mtu au watu watakaowasaidia kutekeleza majukumu yao kwenye maeneo yao ya utawala, ikiwemo yale ya kutatua mizozo ya kifamilia, kijamii, makundi ya kijamii nakadhalika.
Isitoshe, machifu na manaibu wao wako na jukumu la kuzuia uhalifu na ukiukaji wa sheria kutekelezwa kwenye sehemu zao za utawala, kuwatambua wahalifu na kuhakikisha wamekamatwa na kuzuiliwa kituo cha polisi, kufikishwa mahakamani na kuacha sheria ichukue mkondo wake.
Machifu pia wanatarajiwa kutekeleza jukumu la kukabiliana na pombe haramu, kuzuia raia kuficha au kumiliki silaha kama vile bunduki kinyume cha sheria.
Machifu huzuia uharibifu wa misitu kwa kuhakikisha miti au misitu haikatwi kiholela, kuzuia kusambaa kwa maradhi hatari, iwe ni yale ya binadamu au hata wanyama miongoni mwa majukumu mengine mengi.
Machifu, hasa wale wa jinsia ya kike Lamu pia walilalamika zaidi kwa kile wanachosema ni kubaguliwa kijinsia, ambapo raia huwaona kuwa ni viumbe dhaifu na wasio na uwezo au sauti ya kutatua mizozo fulani.
“Utapata mbali na kuona cheo chako cha chifu au naibu chifu kuwa kidogo, pia raia anakuangalia wewe chifu wa kike, kukukadiria na kukupasisha kwamba huwezi kamwe kutatua shida yake,” akasema mmoja wa machifu wa kike wa Lamu aliyedinda kutajwa jina lake.
Aliongeza, “Hapa chao cha chifu kinaonekana cha chini. Ukiwa mwanamke basi ndio sana. Wanakudharau na kukuona kuwa ni mtu usioweza kutatua mizozo yao. Yaani sisi wanawake wanatuona ni viumbe dhaifu machoni mwao, hivyo kuishia kutafuta huduma kwa machifu wenzetu wa kiume au hata kwenda kwa naibu kamishna au kamishna wakidhania kuwa huko ndiko watapata utatuzi.”
Akijibu malalamishi ya machifu dhidi ya kudharauliwa na baadhi ya raia, Kaimu Kamishna wa Kaunti ya Lamu Charles Kitheka alisisitiza kuwa lazima afisi hizo za machifu, manaibu wao, wazee wa mitaa na hata wanachama wa Nyumba Kumi kuheshimiwa vilivyo.
Bw Kitheka aliweka wazi kuwa mpangilio uliopo katika idara ya usalama na utawala nchini ni muhimu na kwamba haufai kukiukwa.
Kaimu Kamishna huyo aliwahimiza wananchi kuzingatia itifaki zinazofungamana na ofisi za utawala Lamu na nchini kwa jumla kila wanapotafuta usaidizi au huduma sehemu hizo.
“Ningewashauri wananchi wetu watukufu kuheshimu itifaki zote zinazofungamana na afisi za utawala Lamu na nchini. Lazima waheshimu vitengo vyote, kuanzia kile cha chini kabisa hadi kile kinachoonekana kuwa cha juu,” akasema Bw Kitheka.
Alisema ili kuona kwamba heshima inazingatiwa na kudumishwa katika ofisi zote za utawala, wamehakikisha mwananchi yeyote anayekaidi itifaki zilizopo anarudishwa kuko huko chini anakokwepa ili kutafuta usaidizi na kutatuliwa shida zao.
Alisisitiza kuwa sio tu wananchi kuelekezwa kwa afisi za machifu bali mara nyingine hata wamerudishwa kutatua mizozo yao kwa wazee wa mitaa baada ya kukimbilia afisi za juu.
“Vitengo vyote vya utawala lazima viheshimiwe. Waanze na nyumba kumi, wazee wa mitaa, manaibu wa chifu na machifu. Ikishindikana kabisa huko ndio wanaweza sasa kufikiria kuzuru afisi za manaibu wa kamishna au kwa kamishna. Hakuna vile mtu ataruka kitengo fulani cha utawala na atarajie kwamba atasikilizwa au kusaidiwa katika ngazi ya juu,” akasema Bw Kitheka.