Walioangamia katika ajali Nyakach sasa ni tisa
CHARLES WASONGA Na ANGELINE OCHIENG
WATU wawili zaidi wameaga dunia kufuatia majeraha waliopata wakati wa ajali iliyotokea eneo la Nyakach na kufanya idadi ya walioangamia kufika tisa.
Afisa Mkuu Mtendaji wa Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga (JOOTRH) Richard Lesiyampe amesema Alhamisi kwamba mbali na watu saba walioangamia eneo la ajali, abiria mmoja aliaga dunia mara baada ya kufikishwa JOOTRH naye wa pili akafariki wakati alikuwa akipokea matibabu.
Mnamo Jumatano, taarifa kutoka kwa kituo cha polisi cha Pap Onditi ilisema ajali hiyo ilitokea katika eneo la Nyalunya, eneobunge la Nyakach, kaunti ya Kisumu katika barabara ya Katito kuelekea Kendu Bay.
Matatu iliyokuwa ikitoka Kisumu mwendo wa saa kumi na moja za jioni iligongana na lori ambalo lilikuwa likisafirisha mchanga wa ujenzi.
“Polisi wa trafiki kutoka kituo cha polisi cha Pap Onditi wameanzisha uchunguzi kuhusu ajali hiyo mbaya iliyochangia watu saba kufa mnamo Februari 21, 2024 saa kumi na moja jioni katika eneo la Nyalunya kando ya barabara ya Katito-Kendu Bay. Hii ni baada ya matatu yenye uwezo wa kubeba abiria 14 kugongana na lori moja,” akasema taarifa kutoka Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) iliyotumwa kwa vyombo vya habari.
Ajali hiyo inatokea mwezi mmoja baada ya basi la kampuni ya Metro lililokuwa likisafiri kutoka Uganda kuenda Nairobi kuhusika katika ajali katika eneo la Ahero na kusababisha vifo vya watu 11.