Habari za Kaunti

Wamuratha aandaa timu ya wanawake 100 kunasua vijana kwa ulevi

March 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA LAWRENCE ONGARO

MBUNGE Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Kiambu, Anne Wamuratha, amefanya kikao maalum na wanawake 100 mjini Thika, ambao lengo lao ni kuhamasisha vijana kujinasua kutoka kwa ulevi na matumizi ya dawa za kulevya.

Bi Wamuratha alisema vijana wanastahili kuhamasishwa kuepuka matumizi ya dawa za kulevya, unywaji wa pombe kiholela na kujihusisha na vikundi viovu.

Mbunge huyo alisema imebainika kuwa vijana wengi wana msongo wa mawazo na matatizo ya akili kutokana na wao wenyewe kujiharibia maisha kupitia kwa uraibu wa vileo na mihadarati.

“Akina mama mashinani wamejitolea kuhamasisha vijana vijijini na mijini kwa lengo la kuwarudisha kwa laini,” alisema Bi Wamuratha.

Alisema wanawake wana nafasi nzuri ya kuwafikia vijana mashinani.

Alikiri mtoto mvulana anahitaji kuangaliwa katika jamii kwa sababu kwa kutelekezwa, amezama sana kwa ulevi na utumizi wa dawa za kulevya.

“Lengo langu kuu ni kuona ya kwamba vijana wanapewa hamasisho halafu wageuze mienendo yao. Lengo pia ni warudi kwa laini kisha watafutiwe miradi tofauti ya kufanya,” akasema.

Alisema wale wanaolengwa sana ni waliokamilisha elimu ya Kidato cha Nne na hawana lolote la kufanya mitaani kwa kukosa kujiunga na vyuo na taasisi mbalimbali za mafunzo.

 

Baadhi ya wanawake walioletwa pamoja na Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kiambu Bi Anne Wamuratha kwa lengo la kuwahamasisha vijana dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya mnamo Machi 18, 2024. PICHA | LAWRENCE ONGARO

Mbali na vijana kuangaliliwa maslahi yao, pia wanawake nao watatafutiwa miradi ya kujiinua kiuchumi.

“Mimi kwa uwezo wangu nitafanya juhudi kuwanunulia akina mama katika makundi yao mahema na viti ili nao waweze kupeana kwa ada kwenye hafla za mazishi na harusi,” alisema mbunge huyo.

Bi Annah Nyambura Mwangi ambaye ni mmojawapo wa wanawake mjini Thika watakaoshughulika na vijana mitaani, alipongeza hatua ya mbunge huyo ya kuwajali vijana.

Alisema pia tabia ya vijana kunywa pombe katika kikombe kimoja ni hatari kwa afya zao.

“Hivi majuzi kijana mmoja alipoteza maisha yake baada ya kuugua maradhi ya kifua kikuu (TB),” alisema Bi Mwangi.

Alisema kikundi chao cha wanawake kitafanya juhudi kutafuta vijana waliozama kwa uraibu wa pombe ili kuwahamasisha.

Alisema vijana wanastahili kutafutiwa kazi ya kufanya badala ya kujihusiaha na ulevi, dawa za kulevya na vikundi viovu.