Wanachama wa Utheri Sacco wapoteza Sh48 milioni kwa usimamizi mbaya Kirinyaga
WAKULIMA kutoka eneo bunge la Gichugu, Kaunti ya Kirinyaga wamefurusha uongozi wa ushirika wa Utheri Sacco.
Wakulima hawa wamejawa na hasira wakidai wamepata hasara ya Sh48 milioni mikononi mwa viongozi wao.
Sasa, wanataka sheria ichukue mkondo na washukiwa washtakiwe wakati ukaguzi wa haraka unafanywa.
Wakulima hao wenye ghadhabu waliongozwa na Bw Stephen Kaunda kushinikiza maafisa hao kuondoka.
Wakizungumza wakati wa mkutano wa dharura ulioitishwa na Waziri wa Biashara na Vyama vya Ushirika Kaunti ya Kirinyaga Calbert Njeru, wakulima hao pia waliwachagua maafisa wa muda ambao watachukua usukani wa Sacco hiyo kwa muda wa siku 90.
Bw Kaunda amewatuhumu viongozi hao kwa kuiba fedha za wanachama wakati wanazongwa na hali ngumu ya maisha kukidhi mahitaji yao ya kila siku.
Anasema wanachama wamelemewa kuendesha familia zao na kulipa karo ya shule kwa kuwa akaunti zao za fedha zimefyonzwa.
Viongozi wakiongozwa na kiongozi wa wengi wa Kirinyaga Muriithi Kibinga wamekashifu usimamizi mbovu wa vyama vya ushirika mbalimbali katika eneo hilo, wakitaka viongozi kuwajibika.
Waziri wa Biashara alisema kuwa maafisa wake watakuwa uwanjani ili kuhakikisha kuwa hakuna hata senti moja ya wakulima itakayoibwa.
“Kulingana na wanachama, chama hiki kimekuwa kikitoa mikopo bila kufuata sheria za chama,” alieleza Bw Kibinga. “Ni muhimu chama hiki kisajiliwe upya kuendana na Katiba ya Kenya.”