• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Wanafunzi wajeruhiwa wakipinga kuhamishwa mwalimu mkuu

Wanafunzi wajeruhiwa wakipinga kuhamishwa mwalimu mkuu

NA WYCLIFFE NYABERI

WANAFUNZI watatu wa Shule ya Upili ya Gianchere Friends katika eneobunge la Nyaribari Chache, Kaunti ya Kisii wanauguza majeraha ya goti baada ya kushtushwa na polisi wakati wa maandamano yao mnamo Alhamisi.

Wanafunzi wa shule hiyo walitoka shuleni wakiandamana kulalamikia uamuzi wa Tume ya Kuajiri Walimu Nchini (TSC)  kumhamisha mwalimu wao mkuu Bw David Obonyo hadi katika shule nyingine.

Kama njia mojawapo ya kuonyesha kutoridhishwa na hatua ya TSC, wanafunzi walifunga barabara kuu ya Kisii-Keroka.

“Ikiwa hakuna Obonyo, hakuna kufunzwa,” ilisikika sauti ya kiimbo kutoka kwa wanafunzi waliokuwa wakiandamana.

Walienda hadi makao makuu ya eneobunge hilo katika kituo cha kibiashara cha Keumbu, kutaka kusikilizwa na maafisa wa elimu lakini walipofika, walikutana na polisi wa kupambana na ghasia ambao waliwatawanya.

“Wanafunzi hao hawakupigwa na polisi kama watu wanavyodai. Lakini waliogopa tu kutokana na risasi za mpira zilizofyatuliwa hewani. Hiyo ndiyo habari ambayo nimepewa na Kamishna Msaidizi wa Keumbu (ACC) ambaye alikuwa huko,” kamanda wa polisi wa Kisii Charles Kases aliambia Taifa Leo kwa simu.

Kufuatia maandamano hayo, shule hiyo imefungwa hadi Jumanne wiki ijayo na wanafunzi wote wakaambiwa kurudi nyumbani.

Shule hiyo ni ya kutwa lakini ina sehemu nyingine ya bweni.

Iko katika eneo la Gianchere, kando ya barabara kuu ya Kisii-Keroka.

Kwa muda wote wa siku hiyo ya maandamano, maafisa wa elimu, bodi ya usimamizi wa shule hiyo na timu ya usalama ya kaunti ya Kisii ya Kati  walijikita katika mkutano wa kuzungumza jinsi ya kusonga mbele.

“Tumekuwa kwenye mkutano tangu asubuhi na tumezingatia baadhi ya masuala ambayo mmeibua. Nyinyi ni wanafunzi wazuri lakini kwa sasa, tumefanya uamuzi wa kuwaruhusu muende nyumbani. Mtarejea shuleni wiki ijayo Jumanne na tafadhali njoo pamoja na wazazi wenu,” mmoja wa wanabodi ambaye aliwahutubia wanafunzi alisema.

Mkurugenzi wa Elimu wa Kaunti Ndogo ya Kisii ya Kati Cyrus Juma alikataa kuwahutubia wanahabari waliokuwa wamekita kambi shuleni tangu asubuhi.

Aliwaelekeza kwa Mkurugenzi wa Elimu wa Kaunti (CDE) katika mji wa Kisii lakini naye hakuwa afisini wakati wa kuwasili kwa wanahabari.

“Nina habari zote kuhusu wanafunzi waliojeruhiwa lakini tafadhali mnaweza kutafuta taarifa zaidi kutoka kwa CDE,” Bw Juma akasema.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Mkongwe Emilio Nsue aongoza ufungaji mabao robo fainali...

Jamaa ashtuka demu aliyedhani mlokole ni mlevi

T L