• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:50 AM
Wanaomiliki baa wahimizwa kushirikiana na polisi kudhibiti pombe haramu

Wanaomiliki baa wahimizwa kushirikiana na polisi kudhibiti pombe haramu

NA WINNIE ONYANDO

WANAOMILIKI vilabu na baa wameombwa kushirikiana na maafisa wa polisi ili kusaidia kudhibiti uuzaji wa pombe haramu.

Wito huo ulitolewa na naibu kiongozi wa wachache katika Bunge la Kaunti ya Nairobi, Waithera Chege.

Kulingana na Bi Chege ambaye pia ni diwani wa wadi wa Nairobi Kusini, ushirikiano kati ya wanaomiliki biashara kama hizo na polisi utasaidia pakubwa kumaliza uuzaji wa pombe haramu.

“Leo nimekutana na wenye vilabu na baa katika eneo langu. Walinieleza kwamba hawajakuwa wakifanya biashara kutokana na agizo lililotolewa na Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja na ndio maana nimekuja hapa ili kuangalia jinsi tunavyoweza kusonga mbele,” akasema Bi Chege.

Mkutano huo wa Bi Chege unajiri siku chache tu baada ya Gavana Sakaja kuamuru baa zote zinazohudumu karibu na vituo vya magari ya uchukuzi zifungwe.

Bi Chege hata hivyo alisema anaunga mkono agizo hilo la Bw Sakaja ila akasema kuwa kuna haja mazungumzo yafanywe.

“Ikiwa baa zitaendelea kufungwa, visa vya uwizi vitaendelea,” akasema Bi Chege.

Kwa upande mwingine, baadhi ya wafanyabiashara katika wadi hiyo wamekubali kushirikiana na maafisa wa polisi.

“Naunga mkono pendekezo hilo. Hii itatusaidia kuendeleza biashara zetu huku tukifuata sheria,” akasema Moses Kimani, mmiliki wa baa katika eneo la Nairobi Kusini.

Naibu wa Rais, Rigathi Gachagua anaongoza katika vita dhidi ya pombe haramu nchini na ameagiza idara ya polisi kutolegeza kamba oparesheni hiyo.

Februari 2024, maafa ya watu wasiopungua 20 yaliyosababishwa na pombe haramu na hatari yaliripotiwa Kirinyaga, jambo lililochangia serikali kukaza kamba msimamo wake.

 

  • Tags

You can share this post!

Raila ana sapoti ya marais wa EAC, Ruto afichulia wabunge...

Watu watatu waangamia katika mkasa wa moto South B

T L