Habari za Kaunti

Wanaume wanajisi wahukumiwa vifungo Uasin Gishu

June 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

Na TITUS OMINDE

WANAUME watatu waliopatikana na hatia ya kunajisi watoto katika maeneo mbalimbali kaunti ya Uasin Gishu wamehukumiwa kifungo cha miaka 30, 20 na 10 mtawalia.

Visa hivyo vilitekelezwa mwaka wa 2016, 2021 na 2022.

Hakimu Mkuu wa mwandamizi wa Eldoret Richard Odenyo aliwafunga wanaume hao mnamo Jumatano baada ya upande wa mashtaka kuthibitisha wana hatia kinyume na makosa ya ngono ya mwaka wa 2006.

Josphat Garo Ichayo ambaye alinajisi msichana wa shule ya chekechea mwenye umri wa miaka sita kutoka Kaunti ndogo ya Turbo, alihukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 30 jela.

Mshtakiwa mwingine, Gilbert Kipkogei Mutai, alipewa kifungo cha miaka 20 baada ya kupatikana na hatia ya kumnajisi mtoto wa miaka 10 mnamo Agosti 7 katika kijiji cha Chepkeno katika Kaunti ndogo ya Ainabkoi.

Mahakama hiyo pia ilimhukumu Francis Simiyu Shikuku, miaka 10 kwa kumshika kwa nguvu msichana wa miaka 17 kati ya mwezi wa Januari na Februari 19, 2016 katika kijiji cha Kipsangui mpakani Kakamega na Kaunti ya Uasin Gishu.

“Mshtakiwa hajutii matendo yake kwani ameendelea kutetea matendo yake tu,” alisema Bw Odenyo alipokuwa akimuhukumu mmoja wa washtakiwa.

Wakati wa kusikizwa kwa kesi hizo mahakama iliambiwa kwamba watatu hao waliwashawishi watoto hao kwa njia tofauti kabla ya kuwanajisi.

“Kesi za unajisi zinazowalenga wasichana wadogo zazidi kuongezeka katika eneo hili, naomba mahakama itoe adhabu kali kwa washtakiwa ili iwe funzo kwa wahusika wa vitendo hivi viovu,” wakili wa serikali aliiambia mahakama.

Washtakiwa wana siku 14 kukata rufaa.