• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Wanawe pasta ni miongoni mwa waliokumbana na ajali wakienda maombi

Wanawe pasta ni miongoni mwa waliokumbana na ajali wakienda maombi

NA FLORAH KOECH

SAA mbili asubuhi mnamo Jumapili, vijana zaidi ya 20 kutoka Kanisa la Kabukoki Revival lililoko Salabani, Baringo Kusini walikutana katika fukwe za Ziwa Baringo kuabiri boti kuhudhuria mkutano wa injili katika Kisiwa cha Kokwa.

Millicent Lekimanti,27, ndiye mtu mzima aliyekuwa amepewa jukumu la kuandamana na vijana hao wa umri wa kati ya miaka tisa na 17.

Vijana hao walikuwa na furaha ambapo waliimba mara tu chombo chao kilipong’oa nanga saa nne asubuhi. Miongoni mwao, walikuwepo watoto wanne wa pasta wa vijana.

Hawakufika katika eneo walilonuia kufika kwa sababu walikumbana na ajali ya boti katika ziwa.

Taifa Leo iliwapata manusura waliosimulia ajali iliyowapata wakielekea Kokwa.

Boti iliyokuwa imewabeba wasafiri 23 ambapo 21 walikuwa wanafunzi wa shule za msingi na shule za upili, ilizama baada ya saa moja tu ya safari.

Elvis Kikenyi,16, ambaye ni mwanafunzi wa Kidato cha Pili, alisema propela ya boti ilishikwa na neti ya kuvua samaki na injini ikafeli.

Wakati mwendeshaji boti alijaribu kuondoa neti hiyo, mawimbi mazito yalisababisha ikapinda.

Wasiwasi uliwaingia na vijana wengi wakaruka kuondoka kwa boti. Haya ni kwa mujibu wa Kikenyi ambaye alipelekwa katika Kisiwa cha Kokwa baada ya kuokolewa.

“Boti lilipopinduka, wote waliokuwa ndani isipokuwa wanne miongoni mwetu, waliruka nje. Tulishikilia kwa sehemu ya injini na dakika chache baadaye, boti jingine kutoka Kisiwa cha Kokwa iliwasili na waliokuwemo wakaanza shughuli za uokozi,” Kikenyi akasimulia.

Watoto wanne katika boti hilo walikuwa wa pasta wa vijana Jane Kikenyi– mmoja wa kiume na watatu wa kike. Mvulana alinusurika lakini mmoja wa kike aliaga dunia. Hata hivyo, wawili bado haijulikani waliko.

Pasta Kikenyi alieleza kwamba kanisa lake huendesha mpango wa kufanya ushirikiano na kanisa jirani lililoko katika Kisiwa cha Kokwa ambapo vijana wa makanisa yote mawili hukutana mara moja kwa mwezi kwa maombi.

Vijana kutoka Kokwa walikuwa wamewatembelea wenzao wa Kabukoki wakati wa likizo ya Pasaka na Jumapili ya mkasa, ndio iliokuwa zamu yao kuenda kisiwani kabla ya shule kufunguliwa.

“Nilifaa kusafiri na vijana wa kanisa letu lakini Askofu aliitisha mkutano mjini Kabarnet Jumapili iyo hiyo,” akaeleza Pasta Kikenyi.

Mwenzake wa Kokwa pia alihudhuria mkutano wa Askofu. Mwanachama wa kanisa lake alimpigia simu akimfahamisha kuhusu ajali iliyotokea.

Mapasta hao wawili waliomba ruhusa na kuondoka na kusafiri kwa gari hadi Kampi Samaki ambapo walipata shughuli za uokozi zikiendelea ziwani.

“Niliona mwili wa mtoto mmoja ukiwa umebebwa na maafisa wa Shirika la Msalaba Mwekundu na nilipodadisi kuhusu mavazi, nilishuku ulikuwa wa binti yangu,” akaeleza.

Baadaye alitambua mwendazake alikuwa binti yake wa umri wa miaka 12 ambaye alikuwa mwanafunzi wa Gredi ya Sita.

Kufikia Jumatatu usiku, watu 17 waliokuwa kwa boti hilo walikuwa wameokolewa, akiwemo mvulana kifungua mimba wa pasta, ambaye ni mwanafunzi wa Kidato cha Pili.

Watu sita walikuwa bado wanakosekana, wakiwemo wasichana wawili wa pasta. Shughuli za uokozo zilikuwa zikiendelea.

“Ni huzuni kupoteza watoto watatu kati ya wanne,” akasema pasta huku machozi yakimtoka.

Wasichana wake ambao hawajapatikana ni wa Kidato cha Kwanza na Gredi ya Nne mtawalia.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Kamata Linturi ikiwa unataka kujitakasa kuhusu mbolea feki,...

Maandamano Kiganjo kupinga ‘udhalimu’ wa kanjo wa Kiambu

T L