• Nairobi
  • Last Updated June 15th, 2024 1:54 PM
Washukiwa watatu wa wizi wauawa Industrial Area

Washukiwa watatu wa wizi wauawa Industrial Area

NA MWANGI MUIRURI

WASHUKIWA watatu wa wizi wamepigwa risasi na kuuawa na maafisa wa polisi katika barabara ya Lusaka eneo la Industrial Area, Kamanda wa polisi Nairobi Bw Adamson Bungei amesema.

Watatu hao, ambao aliwataja kuwa wanaume wa umri wa ujana, alisema walipigwa risasi Jumatano alfajiri.

“Watatu hao walifumaniwa na polisi wakiwavamia wananchi waliokuwa wakielekea kazini. Walikuwa wakipora watu mali zao kama pesa, simu na mikufu,” akasema Bw Bungei.

Alisema kwamba kwa muda, eneo hilo limekuwa likitatizika kwa utovu wa usalama unaosababishwa na wahalifu wa kutumia pikipiki kufika kwa waathiriwa na kisha kutoroka baada ya kutekeleza uhalifu huo.

“Hapo ndipo tuliweka mikakati na maafisa wetu wakajitokeza eneo hilo wakijifanya wapitanjia na ndipo baadhi yao wakajipata wakivamiwa na vijana hao. Kulishuhudiwa mshikemshike polisi walipojitambulisha na wakawaagiza wahalifu hao wajisalamishe lakini wakakataa. Mmoja wao alitwaa bunduki na akafyatua risasi akiwalenga maafisa na ndipo walijibiwa kwa nguvu sawa na wakaangamizwa,” akasema.

Alisema bunduki aina ya Ceska ikiwa na risasi nane ilitwaliwa kutoka kwa washukiwa hao wa uhalifu.

Bw Bungei alisema kwamba washukiwa hao pia mnamo Jumatatu walikuwa wamevamia raia wa asili ya Kihindi na kumpora Sh12,000 pamoja na mkufu wa dhahabu.

“Vijana hao walitorokea katika mmojawapo wa mitaa ya mabanda ya Mukuru ambapo maafisa waliokuwa wakiwakimbiza waliwakosa. Lakini mnamo Jumatano, siku zao arubaini zilitimia,” akasema.

Miili ya washukiwa ilipelekwa hadi mochari ya City ambapo itafanyiwa uchunguzi zaidi wa kuwatambua.

  • Tags

You can share this post!

Nyanya mshukiwa wa ukahaba anaswa Thika

Maswali ya KCSE kuhusu mada ya ‘Ngeli za Nomino’

T L